Thursday, December 31, 2020

HAKI MADINI YATOA MAFUNZO KWA WACHEKECHAJI

Meneja miradi wa shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini Emmanuel Mbise akizungumza na wachekechaji wanaochekecha ndani ya ukuta unaozunguka madini ya Tanzanite.

Wadau wanaochekecha migodi ya madini ya Tanzanite wakiwa kwenye mafunzo ya usalama kazini yaliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini.
*********************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Haki Madini la jijini Arusha, limewajengea uwezo wachekechaji wanaochekecha udongo ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite, kwa kuwapatia elimu ya namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na shughuli wanazofanya.
Ofisa miradi wa shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise akizungumza kwenye kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro amesema lengo ni kuwajengea uwezo zaidi wa kufanya kazi katika mazingira salama.
Mbise amesema katika kufanya kazi za uchekechaji inatakiwa kuvaa vifaa vya kujikinga na vumbi ili kuondokana na ugonjwa wa kifua kikuu na ulanga kuingia kwenye kifua.
“Wakati wa kuchekecha muwe mnamwagia maji katika udongo ili vumbi lisiingie vifuani na kwenye mapafu kisha kupata TB na Silikosisi kupitia vumbi na ulanga unaokuwepo wakati wa kazi,” amesema Mbise.
Amesema kufanya kazi kwa muda mrefu hujenga majeraha kwenye baadhi ya viungo vya mwili na mifupa hivyo tunapaswa kupumzika kila baada ya kzii na kufanya mazoezi.
“Pia kwenye shughuli zetu hizi za uchekechaji wa madini tunapaswa kupumzika ili kuupa mwili nafasi kwani madini yapo tuu yanatakiwa yatupe faida na yasituathiri,” amesema Mbise. 
Ofisa mtendaji wa kata ya Naisinyai, Valentine Tesha amewataka wachekechaji hao 60 waliopatiwa mafunzo hayo wawe mabalozi wazuri kwa kutoa elimu waliyoipata kwa wengine ambao hawakuipata.
Tesha amesema washiriki hao wakisambaza elimu hiyo kwa baadhi ya wachekechaji ambao hawajafika kwenye mafunzo hayo watakuwa nao wamejengewa uwezo.
Mmoja kati ya wachekechaji hao, Isaya Maliyaki amesema wamekuwa wakitoa elimu waliyoipata kwa baadhi ya vijana wachekechaji ila hawatekelezi.
Maliyaki amesema baadhi ya vijana walevi wanawaeleza kuwa watumie vifaa vya kujikinga vumbi kwa kuvaa barakoa lakini hawatekelezi hilo.
Mwenyekiti wa wachekechaji ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite, Nai Leyani amelishukuru shirika la Haki Madini kwa kuwapa elimu hiyo kwani kwa namna moja au nyingine imewasaidia.
Leyani amesema wamekuwa wakiwapa elimu baadhi ya wachekechaji wenzao ambao hawajapata mafunzo hayo hasa wanawake ambao wamekuwa wanatekeleza hayo kwa kuvaa vifaa vya kujikinga na vumbi na kumwagia maji mchanga.

 

No comments :

Post a Comment