Alhamisi, 24 Disemba, 2020 Dar es Salaam, Tanzania.
Washindi
wa kwanza wa Tuzo za Kidigitali (Tanzania Digital Awards) mwaka 2020
wametangazwa rasmi baada ya watanzania kupiga kura.
Jumla
ya wawania tuzo 50 wameibuka washindi katika jumla ya vipengele 50
kutoka katika makundi tisa ikiwemo kundi la Serikali Mtandaoni,
Maendeleo na Diplomasia Mtandaoni, Masoko Mtandao, Burudani Mtandaoni,
Vyombo vya Habari Mtandaoni, Uvumbuzi wa Kidijitali, Mawasiliano ya
Kidijitali, Uchechemuzi Mtandaoni na Tuzo ya Ujumla ya Chaguo la Watu.
Tuzo
hizi zilizinduliwa nchini kwa mara ya kwanza mnamo Januari 16, 2020 kwa
lengo la kutambua juhudi za watu binafsi, mashirika, kampuni na hata
Serikali katika kutumia teknolojia ya kidigitali kuleta mabadiliko
chanya katika jamii. Baadhi ya walioshinda vipengele vingi ni pamoja na
Diamond Platnumz ambaye ameshinda vipengele vitatu ikiwemo kipengele cha
Tuzo ya Ujumla, Msanii bora wa mwaka na mraghibishi wa mwaka. Millard
Ayo pia ametwaa tuzo tatu, tuzo ya kiongozi bora wa vyombo vya habari
vya mtandaoni, TV bora ya Mtandaoni na Blog bora ya Mtandaoni.
Taasisi
zilizonyakua tuzo nyingi ni pamoja na Ubongo Kids na Idara ya Uhamiaji
–kila mmoja tuzo mbili. Ubongo Kids wametwaa tuzo tuzo ya ukurasa bora
wa elimu mtandaoni na tuzo ya aplikesheni bora ya elimu mtandaoni. Idara
ya Uhamiaji wametwaa tuzo ya uvumbuzi bora kupitia huduma yao ya kutoa
hati ya kusafiria kielektroniki. Uhamiaji pia wameshinda tuzo ya taasisi
bora ya Serikali mtandaoni.
Vodacom
Tanzania imeibuka na tuzo mbili baada ya aplikesheni yake ya M-PESA
kuzawadiwa kama Aplikesheni Bora ya Huduma za Kifedha. Tuzo nyingine
iliyoenda kwa Vodacom ni tuzo ya Kampeni Bora ya Masoko Mtandaoni ambapo
Vodacom wameshinda kupitia kampeni yake ya ‘Yajayo Yanafurahisha’.
Tuzo
ya heshima imekwenda kwa Muhidin Issa Michuzi ambaye ametambuliwa kama
kiongozi bora wa vyombo vya habari mtandaoni kwa kuanzisha na kuendeleza
vyombo vya habari kwa njia ya mtandao nchini Tanzania.
Baada
ya kutangaza orodha ya washindi, Mkuu wa Programu, Utafiti na Uvumbuzi
wa Serengeti Bytes, Ndugu Genos Martin amesema kwa kiasi kikubwa tuzo
hizi ziliathiriwa na mlipuko wa Covid-19 uliojitokeza mara baada ya
kuzinduliwa kwa tuzo hizo. Hata hivyo, Martin anakiri kwamba Covid-19
kwa kiasi fulani imesaidia kuweka msisitizo wa namna ambavyo teknolojia
za kidijitali haziepukiki katika maisha ya sasa na hivyo kufanya tuzo za
Tanzania Digital Awards kuwa na maana zaidi.
‘’Mara
baada ya kutangaza tuzo hizi kwa mara ya kwanza mwezi Januari tulipata
mwitikio mkubwa sana wa watu na makampuni na hata taasisi za serikali na
wadau wengine kujitokeza kushiriki. Kuingia kwa mlipuko wa Covid-19
nchini kumeathiri kwa kiasi kikubwa maandalizi ya tuzo hizi. Hata hivyo,
Corona haijaharibu pekee bali kwa upande mwingine imeonesha wadau na
hata sisi waandaaji kwamba matumzizi ya teknolojia za kidigitali ndio
mtindo mpya wa maisha hivyo tuzo hizi zimekuja wakati sahihi na kila
mmoja anapaswa kuziunga mkono”. – amesema Martin.
Akizungumzia
kuhusu washindi, Martin amesema washindi wote wa tuzo za Tanzania
Digital Awards wamestahili kushinda hasa kwa kutazama mambo makubwa
wanayoyafanya kupitia majukwaa ya kidigitali. Martin amefafanua kwamba
mwakani tuzo hizo zitatanuliwa zaidi kuhakikisha watu wengi zaidi
wanashiriki na kila sekta inaguswa kwa lengo la kuchochea ubunifu na
uvumbuzi katika kukuza maendeleo ya teknolojia za digitali nchini
Tanzania.
“Tunawapongeza
washindi wote kwa kupigiwa kura nyingi katika vipangele walivyowania,
washindi wote wamestahili ushindi kwa kutazama juhudi zao katika
majukwaa ya kidigitali. Tunaamini ushindi wao utachochea ubunifu na
uvumbuzi katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii na taifa kwa
ujumla. Katika tuzo zijazo tutahakikisha wadau wengi zaidi wa teknolojia
za kidigitali kutoka katika sekta zote wanapata taarifa na kushiriki
kikamilifu”,amesema Martin.
Tuzo
za Tanzania Digital Awards zilizunduliwa rasmi Januari 16, 2020 kwa
lengo la kuwatambua watu, taasisi na kampuni zinazotumia teknolojia za
kiditali kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Tanzania Digital Awards
zinalenga kuchagiza Uwajibikaji, Ubunifu na Uvumbuzi kwenye majukwaa ya
Dijitali. Zikiwa katika Makundi tisa na zaidi ya vipengele vidogo 50,
tuzo hizi ni za kwanza na kubwa zaidi kutambua juhudi zinazofanyika ili
kuleta mapinduzi ya kidijitali Tanzania na nje ya mipaka.
Katika
msimu wa kwanza, yalifanyika mapendekezo ya wawania tuzo zaidi ya 54,
034 huku kura zaidi ya 100,000 zikipigwa katika vipengele 50.
Kwa taarifa zaidi tembelea
No comments :
Post a Comment