**********************************
Na Mwandishi wetu Arusha
WAJASIRIAMALI na
wadau wa maendeleo wametakiwa kuwekeza kwenye dhamana za serikalini ili
wapate faida wao wenyewe na serikali kwa ujumla kuliko kutegemea miradi
mingine ikiwemo nyumba za kupangisha.
Pamoja na kupata
faida binafsi pindi wakiwekeza kwenye dhamana hizo, serikali pia
itanufaika kwa kutumia fedha hizo za uwekezaji katika kujenga na
kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii.
Kamishna msimamizi wa
madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Lekinyi Mollel ameyasema hayo
jijini Arusha, wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa ujasiriamali
kwenye semina ya kuwajengea uwezo.
Mollel amesema pamoja na kuwekeza katika dhamana za serikali fedha za wajasiriamali hao hazitakuwa kwenye viashiria hatarishi.
Amesema huu ni wakati
muafaka kwa wajasiriamali, wenye viwanda, wafugaji, wakulima, wadau wa
madini na sekta nyingine kuwekeza kwa wingi kwenye dhamana za serikali.
Katibu Tawala wa mkoa
wa Arusha, Richard Kwitega amesema wananchi wanaponunua dhamana hizo za
serikali hupata faida baada ya vipindi mbalimbali ikiwemo miezi sita na
mwaka mmoja.
Kwitega amesema
dhamana hizo za serikali ni rafiki kwani mwekezaji ana uhuru wa kuuza
dhamana sake muda wowote akihitaji kufanya hivyo.
Mkuu wa kitengo cha
mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja
amesema uanzishwaji wa minada ya dhamana za serikali ni mkakati wa
kuendeleza masoko ya fedha nchini.
Mwaipaja amesema
dhamana za serikali zimegawanyika katika makundi mawili ya dhamana za
muda mfupi isiyozidi mwaka mmoja na hatifungani zinazotumiwa na serikali
za miaka miwili hadi 20.
Katibu mkuu wa
wafanyabiashara wa madini, Noel Olevaroya amesema atakuwa balozi mzuri
kwa wachimbaji madini na wafugaji katika kufikisha elimu ya uwekezaji wa
dhamana za serikali.
“Sisi wafanyabiashara
wa madini tuna uwezo wa kuwekeza katika dhamana hizo na pia wafugaji
tuna mifugo mingi hivyo ili kufuga kitaalamu tutaifikisha elimu hii
kwao,” amesema Olevaroya.
Mjasiriamali Theresia
Onesmo amesema kupitia elimu hiyo ya uwekezaji kwenye dhamana za
serikali ataachana na mpango wa kujenga nyumba za kupangisha na kuwekeza
kwenye dhamana za serikali.
No comments :
Post a Comment