Friday, December 4, 2020

Umuhimu wa wastaafu kununua dhamana za serikali za muda mrefu-I.

Meneja Uhusiano na Itifaki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Zalia Mbeo

Majira Ijumaa 04 Desemba 2020

Katika sehemu ya kwanza na ya pili tulizungumzia kuhusu dhamana za muda mfupi au hatifungani za muda mfupi na tuliona faida zake mbalimbali na jinsi gani zinaweza kumuingizia mwekezaji kama vile mstaafu kipato kizuri kisichokuwa na wasiwasi wowote wa jinsi ya kupatikana.

Wiki hii tutaongelea kuhusu dhamana za muda mrefu au hatifungani za muda mrefu kwa mazingira ya nchi ya hapa Tanzania na namna gani zinavyochangia katika kutengeneza kipato kwa wastaafu na kwa wawekezaji wengine, kama anavyoendelea kuelezea MWANDISHI WETU CHRISTIAN GAYA:

Kulingana na Meneja wa Uhusiano na Itifaki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Zalia Mbeo anasema, kwa kawaida BoT, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza dhamana za serikali za muda mrefu, ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka kwa taasisi na kwa mwananchi mmoja mmoja wawekezaji kama vile wastaafu wanaopata mafao yao ya mkupuo.

 “Dhamana za serikali za muda mrefu kwa kiwango kikubwa huiwezesha serikali kugharamia kwa muda, nakisi katika bajeti yake inayosababishwa na upungufu wa mapato ukilinganisha na mapato ya serikali. Dhamana hizi huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani kupitia minada na baada ya hapo uuzaji wa dhamana hizo hufanywa kwenye soko la upili” Zalia anasema.

Meneja wa Uhusiano na Itifaki BoT anataja baadhi ya faida ya ununuzi wa dhamana za serikali ikiwa ni njia mojawapo ya uwekezaji na uzuri wake ni kwamba kuwekeza katika dhamana za serikali ni salama, kwa sababu serikali haitarajiwi kukiuka masharti ambayo ndiyo matarajio na mategemeo ya wadai wake wakati wa malipo.

Kwa upande mwingine ni kwamba dhamana za serikali za muda mrefu zinahamishika na hata mstaafu mwekezaji anaweza kurithisha familia yake, pia mstaafu mwekezaji anaweza kuziuza kabla ya muda wake wa kuiva endapo itakuwa ni lazima afanye hivyo.

Pia dhamana za serikali za muda mrefu zinaweza kutolewa kama dhamana kwa mstaafu kwa ajili ya mkopo kwenye mabenki na taasisi zingine za fedha zinazotoa mikopo.

Siyo hivyo tu dhamana za serikali za muda mrefu zina kiwango cha faida inayoridhisha kwa mstaafu yeyote mwekezaji ukilinganisha na faida zinazotolewa na taasisi zingine za fedha zinazotoa mikopo kwa wastaafu.

Hivyo dhamana za serikali au hatifungani za serikali za muda mrefu ni fursa nzuri ya uwekezaji hasa kwa wale wastaafu wanaohitaji kuwekeza fedha na kupata faida bila kutumia nguvu nyingi au kuwekeza bila kupata hasara hasa kama vile wastaafu na taasisi mbalimbali za fedha.

“Kuna aina mbili ya masoko ya dhamana za serikali za muda mrefu. Soko la awali ni pale ambapo Benki Kuu huuza dhamana hizi kwa mara ya kwanza.

Mnada hufanyika mara mbili kwa mwezi. Uuzaji wa dhamana hizo baada ya hapo hufanywa kwenye soko la upili” Zalia anafafanua zaidi.

Anasema ya kuwa kila mkazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo wastaafu wanastahili kushiriki katika mnada wa dhamana za serikali za muda mrefu.

“Wakala au mwekezaji yeyote mwenye kiwango cha kuanzia shilingi milioni moja (TZS 1,000,000.00) na kuendelea anaruhusiwa kushiriki katika mnada wa dhamana za serikali”, anafafanua.

Anasema kuwa, BoT inao mfumo maalumu wa kuchakata na kuhifadhi taarifa zote za minada ya dhamana za serikali za muda mrefu.

Minada yote ya dhamana hizo hufanyika na kumbukumbu zake huwekwa kwa njia za kielektroniki. Hivyo basi hakuna shahada au hati inayotolewa kwa wawekezaji.

Anafafanua zaidi ya kuwa BoT hutoa dhamana za serikali za muda mrefu na zinazoiva kwa nyakati tofauti.

Kwa sasa dhamana hizi ni huwa ni za miaka  2, 5,7,15 na za miaka 20. Hivyo dhamana za serikali za muda mrefu au hatifungani za muda mrefu ni dhamana zinazoiva katika muda unaozidi mwaka mmoja.

“BoT mara nyingi huwa inatoa tangazo la mpango na utaratibu wa utoaji wa dhamana za serikali za muda mrefu kwa mwaka.

Mpango huu hutolewa kupitia kwenye magazeti na hupatikana pia kwenye tovuti ya BoT. Mpango huo huonesha muda wa dhamana ya serikali itakayotolewa na tarehe ya mnada” anasema.

Washiriki wanapaswa kutumia fomu maalumu za zabuni zinazoitwa CDS/FORM/03 kwa ajili ya kushiriki katika minada ya dhamana za serikali. “Fomu hizi zinapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania na katika ofisi za mawakala waliosajiliwa kama vile taasisi za fedha na mabenki mbalimbali,” Zalia anafafanua zaidi.

Anasema kuwa kiwango cha chini cha kuwekeza kwenye dhamana za serikali za muda mrefu ni shilingi milioni moja tu (TZS 1,000,000.00) zikiwa katika mafungu ya shilingi laki moja (TZS 100,000.00). Bei ya dhamana za serikali za muda mfupi zinapaswa kuwa na tarakimu yenye desimali nne.

Wastaafu wawekezaji na wawekezaji wengine huwa wanawasilisha fomu za zabuni kwa mawakala waliosajiliwa.

“Fomu hizo zilizojazwa zikiwa na saini ya mstaafu mwekezaji au mwekezaji mwombaji huwa zinawasilishwa kwenye ofisi za mawakala walisajiliwa ambao baada ya hapo huwa wanazituma BoT kwa njia ya kielektroniki saa tano kamili asubuhi siku ambayo hutajwa kuwa ndiyo ya mnada wa dhamana hizo,”Zalia anasema.

Anasema pamoja na hayo yote kumbuka ya kuwa BoT ina haki ya kukubali au kukataa fomu mojawapo ya zabuni au zote zilizowasilishwa katika mnada husika.

Kwamba BoT huendesha mnada kwa kutumia mfumo wa kompyuta ujulikanao kama mfumo wa dhamana za serikali “GSS”.

Ili kutambua washindi mfumo huu wa kompyuta hutumia mfumo wa bei tofauti. Kila mzabuni aliyeshinda huwa anawajibika kwa bei aliyopendekeza.

Washindi wa zabuni huorodheshwa kwa kuanzia na mshindi aliye toa bei ya juu zaidi hadi yule aliyetoa bei ya chini mpaka pale ambapo mafungu yaliyotolewa kwa ajili ya mauzo ya dhamana hizo yanamalizika.

Akifafanua zaidi anasema kuwa endapo washindi katika bei ya mwisho watahitaji kiwango cha dhamana zaidi ya kiwango kilichobaki katika mafungu yaliyotolewa.

BoT huwa inawagawia washindi wote kiasi kilichobaki kwa uwiano wa zabuni zao hadi kiwango kilichobaki kinapomalizika.  

Zalia anasema kuwa matokeo ya mnada yanatangazwa kwenye tovuti ya BoT. Na kwamba mawakala waliosajiliwa pia wanaoneshwa matokeo hayo kwenye ofisi zao.

Hivyo wazabuni wanaoshinda huwa wanapatiwa namba za malipo ambazo huwa zinazotolewa na mawakala mara baada ya matokeo ya mnada kutolewa.

“Namba hizo za malipo huwa zinatumika kama namba za marejeo kwa ajili ya kufanya malipo ya dhamana za serikali zilizonunuliwa kwa kupitia mfumo maalumu wa malipo kati ya mabenki ‘TISS,”Zalia anasema.

Anasema kuwa sababu ya ukosefu wa elimu miongoni mwa wastaafu wengi na kwa umma kwa ujumla juu ya soko hili la dhamana za serikali, mara nyingi unakuta mabenki ndiyo, hasa miongoni mwa taasisi zinazowekeza mara kwa mara kwenye hatifungani za serikali yaani dhamana za serikali. Itaendelea wiki ijayo

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com +255 655 13 13 41, unaweza kutembelea www.hakipensheni.blogspot.com, info@hakipensheni.co.tz

 

 

 

No comments :

Post a Comment