Friday, December 18, 2020

TBA YATANGAZA KIAMA WADAIWA SUGU KODI ZA MAJENGO.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo nchini (TBA,) Mbunifu Majengo. Daud Kondoro akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wadaiwa sugu wa kodi za nyumba na majengo yanayosimamiwa na TBA.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mbunifu Majengo  Daud Kondoro (kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wadaiwa sugu wa kodi za nyumba na majengo yanayosimamiwa na TBA, kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wakala TBA, Bw. Said Mndeme.

********************************

NA NAOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) imewataka wapangaji wote wanaodaiwa zikiwemo  taasisi

za serikali kulipa kodi kabla ya mwezi january mwakani ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima ikiwemo kuwatoa katika nyumba hizo.

Imeelezwa kuwa hadi sasa jumla ya fedha shilingi bilioni nne zinadaiwa kwa wapangaji  hao kutoka taasisi mbalimbali zinazotumia nyumba zinazosimamiwa TBA.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa TBA, Mbunifu Majengo Daud Kondoro,  amesema kuwa wapangaji wote zikiwemo taasisi za umma zinatakiwa kuhakikisha wanalipa madeni hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa ikiwemo wapangaji kuondolewa kwenye nyumba hizo.

“TBA imeazimia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wapangaji wote tunaowadai, moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuwaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambao wamepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA” amesema Mbunifu Majengo Kondoro

Amebainisha kuwa tayari wana kampuni mbili za udalali wa Mahakama ambazo ni Yono Auction Mart na Ms.Harvest Tanzania Limited na tayari wamekabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa hatua litafanyika katika Mikoa yote nchini.” amesema Kondoro.

Aidha amesema, katika hatua nyingine ya kuhakikisha fedha hizo zinalipwa ni kuwafungulia mashtaka wadai wote watakaoondolewa katika nyumba na majengo hayo.

Vilevile amewataka watumiaji wengine wa nyumba na majengo yanayosimamiwa na TBA kuendelea kulipa kodi zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa aina yoyote.

Mkurugenzi wa idara ya miliki (TBA,)  Said Mndeme amesema taasisi za Serikali zipatazo 17 zinadaiwa huku makusanyo ya madeni hayo yakielekezwa katika  kusaidia kufanya ukarabati wa baadhi ya nyumba na makazi.

Amesema, TBA imerahisha kufanya malipo kwa wateja wao na sasa malipo hayo yanafanywa kwa njia ya simu na kusema kuwa wataendelea kufanya marekebisho ya nyumba zote katika kila halmashauri nchini.

 

No comments :

Post a Comment