***************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
WAATHIRIKA 10 wa
mikopo umiza wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamerejeshewa mali
zao baada ya kuchukua mikopo umiza hiyo na kuishiwa matumaini ya
kupatiwa mali zao.
Waathirika hao 10 wa
mikopo umiza waliofaidika ni Raphael Ombade aliyerudishiwa gari aina ya
Opel Vectra na kadi yake, Yasintha Adiro nyumba na nakala ya hati ya
kiwanja, Mosses Makala nyumba tatu na kadi ya pikipiki, Bernady Nyarasya
mkataba wa nyumba na Godwin Mmasy pikipiki .
Wengine ni Jimmy
Kibindi pikipiki, John Laizer shamba la ekari tatu na nusu na mkataba wa
kuweka shamba rehani, Mohamed Matinda gari na kadi yake na Lengayen
Rumas gari aina ya Toyota Land Cruser na kadi yake.
Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Joseph Mkirikiti amekabidhi mali hizo Desemba 24 kwenye mji
mdogo wa Mirerani na Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro ambapo mali
hizo zilikamatwa baada ya waathirika wa mikopo umiza kusaidiwa
kurejeshwa na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU).
Mali hizo ni viwanja,
nyumba, pikipiki, magari, mashamba na kadi za pikipiki na magari
zilizokopwa kwa shilingi milioni 32 lakini aliyetoa mikopo umiza hiyo
akawa anawadai marejesho na riba ya shilingi milioni 80.
Mkirikiti ameipongeza TAKUKURU kwa kufanikisha kurejeshwa kwa mali hizo kutoka kwa waathirika wa mikopo umiza.
Amesema japokuwa
waathirika hao wa mikopo umiza walikuwa na mahitaji ya fedha wangepaswa
kukopa kwenye taasisi za fedha kuliko kukopa kwa mtu binafsi ambaye hana
leseni ya kufanya biashara.
‘Kuna taasisi nyingi
za fedha ikiwemo mabenki ambayo yanatoa mikopo kihalali hivyo wananchi
msiwe mnajihusisha kuchukua mikopo ambayo hainamanufaa kwenu kwani
japokuwa mtu utakuwa una shida ya fedha lakini unaangamia,” amesema
Mkirikiti.
Mkuu wa wilaya ya
Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula amempa siku 14 aliyechukua mali
kupitia mikopo umiza hiyo kurudisha mali zilizobakia kwa waathirika hao.
“Naipongeza TAKUKURU
Simanjiro kwani inafanya kazi kubwa ya kuisaidia jamii kwenye masuala
mbalimbali ila wananchi nanyi msikubali kurubuniwa na watu matapeli
kwani kuna hadi viongozi wa dini wanashiriki kufanya hii michezo,’
amesema mhandisi Chaula.
Mkuu wa TAKUKURU
Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ametoa rai kwa watu wenye nia ya
kufanya biashara ya fedha, wafuate utaratibu wa kukata leseni na kulipa
kodi stahiki ili waweze kufanya biashara hiyo kwa mujibu wa sheria.
Makungu amesema baada
ya urejeshaji huo ni vyema wananchi wakafahamu kuwa sheria ya biashara
ya fedha The Microfinance Act 2018 inatoa katazo kufanya biashara ya
fedha kwa kutoza riba bila kuwa na leseni.
“Kifungu cha 16 cha
sheria hiyo kinatoa adhabu kali ya kifungo kisichopungua miaka miwili na
kisichozidi miaka mitano kwa anayekiuka sheria hii,” amesema Makungu,
Mkuu wa Takukuru
wilaya ya Simanjiro Adam Kilongozi ametaja baadhi ya mali zilizokuwa
zimechukuliwa kwenye mikopo umiza hiyo ni magari, pikipiki, nyumba,
mashamba na kadi za pikipiki na magari.
Kilongozi amempongeza
hakimu wa mahakama ya wilaya ya Simanjiro Charles Uisso kwa kutenda
haki na kutoa uamuzi sahihi baada ya kupitia maamuzi ya mahakama ya
mwanzo Mirerani kwani mkopeshaji hakuwa na leseni ya kufanya biashara
hiyo.
Baadhi ya waathirika
wa mikopo umiza hiyo wameishukuru serikali kwa kuingilia kati hadi
kufanikiwa kurejeshewa mali zao kwani ni muda mrefu walichukua mikopo
hiyo na kubambikiwa riba kubwa.
Mkazi wa mji mdogo wa
Mirerani, Yasintha Adiro amesema mume wake Ogola Owende alichukua
mkopo wa shilingi milioni 10 na laki tatu na kuweka rehani nyumba na
hati ya kiwanja kasha akakimbia na kuhama mji huku akiwaachia watoto.
Yasinta amesema
alifungua kesi mahakama ya mwanzo Mirerani na kushindwa kesi hiyo ila
akakata rufaa mahakama ya wilaya ya Simanjiro akapatiwa ushindi kwani
mwenye mikopo umiza huyo hakuwa na nyaraka zinazomruhusu kukopesha watu
hivyo akashinda kesi na kurejeshewa nyumba yake.
Mkazi wa kata ya
Shambarai Mosses Makala amesema nyumba zake tatu zilikuwa rehani na
aliyempa fedha zake shilingi milioni saba na akatakiwa kurejesha
shilingi milini 43 kisha nyumba hizo zikageuzwa kuwa maghala ya
kuhifadhi mahindi huku nyumba moja ikibomolewa.
Hata hivyo, mmiliki
wa mikopo umiza hiyo Nicas Lyimo amesema baadhi ya mali za wakopaji hao
ikiwemo baadhi ya magari zililetwa na wamiliki zikiwa zinavutwa hivyo
hatagharamikia kuzitengeneza zaidi ya kunirudishia kama zilivyo.
“Kuna baadhi ya mali
ikiwemo pikipiki na magari zililetwa kwangu zikiwa zinasukumwa au
kuvutwa na kamba hivyo watarejeshewa zikiwa kwenye hali hiyo zilizokuja
kwani hazikuwa zinatumika zilikaa hapa kama dhamana, naomba hilo
lifahamike,” amesema Lyimo.
Amesema nyumba moja
kati ya tatu za Makala ilibomoka kutokana na mvua zilizonyesha ila
nyingine mbili zipo na alihifadhi mahindi na atayaondoa baada ya amri ya
serikali.
No comments :
Post a Comment