Friday, December 25, 2020

Miradi ya shule ya Shilingi Bilioni 1.15 iliyoshindikana kumalizika yamuibua RC Wangabo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Carolius Misungwi baadhi ya Mifuko 30 ya Saruji ikiwa ni ahadi ya mkuu wa mkoa katika kuunga mkono juhudi za wananchi katika kukamilisha madarasa ya shule za Sekondari Wilayani humo.  Baadhi ya Wananchi na viongozi mbalimbali wakishiriki katika songambele ya ujenzi wa madarasa 7 ya Shule ya Sekondari Matai Wilayani Kalambo.

*******************************************

Serikali kupitia miradi yake ya Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) Pamoja na mradi wa Lipa

kulingana na Matokeo (EP4R) imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa jumla ya kiasi cha Shilingi 1,152,557,008.77/= kwaajili ya kutekeleza ujenzi wa madarasa 18, matundu ya vyoo 178, mabweni mawili kwa shule za Msingi na Sekondari fedha ambayo halmashauri hiyo ilipatiwa tangu mwezi Juni mwaka 2020 lakini hadi kufikia mwezi Disemba 2020 ujezni wake haujafikia hata asilimia 50 ya ukamilishaji.

 

Kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amekemea uzembe unaofanywa na viongozi wa halmashauri hiyo huku akisikitishwa na kitendo cha Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo Msongela Palela kuchukua ruhusa ya kuondoka nje ya mkoani huo huku katika halmashauri yake kukikosekana madarasa saba kwaajili ya wanafunzi 254 waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza katika halmashauri hiyo.

Mbali na fedha za miradi hiyo wananchi wa Kata ya Matai kwa kushirikiana na halmshauri wameanza ujenzi wa vyumba vya madarasa manne katika shule ya Sekondari Matai ambavyo vinatakiwa kukamilika kabla ya tarehe 28.2.2021 kwaajili ya kuwapokea wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa wananfunzi hao wilayani humo.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya shule za Msingi za Sekondari katika Halmshauri hiyo wakati alipokuwa katika Shule ya Sekondari Matai inayotekeleza ujenzi wa madarasa sab ana mabweni mawili Mh. Wangabo alisema kuwa amekosa Imani na utendaji kazi wa halmashauri hiyo baada ya kuona miradi inayogharamiwa na serikali kutomalizika kwa wakati huku miradi inayotekelezwa kwa kushirikiana gharama na wananchi kutokuwa na dalili ya kumalizika.

“Miezi sita lakini watu wanafanya utekelezaji kwa 42% sasa mimi inanipa mashaka,huku tu ambako kuna fedha ujenzi haujakamilika kwa miezi sita, je hukuambako tunaanza msingi nahakuna fedha ni juhudi za wananchi tutakamilisha baada ya muda gani? Ninayasema haya kwa uchungu mkubwa kwasababu angalau mngenitia Imani kwamba ile fedha ya serikali iliyopokelewa Shilingi milioni 756 zilikwisha kamilika na miundombinu yote inaonekana na iko vizuri kwa ubora wake,lakini hakuna tuko  42% hatujamaliza na tuna mzigo mkubwa wa haya madarasa tuko kwenye msingi, Imani kwangu itatoka wapi kwamba huu ujenzi tutaukamilisha ndani ya iezi miwili, ndugu wanachi tutafika?” Alihoji.

Aidha, Aliutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi ya ziada ili kutekeleza maagizo ya serikali ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanaendelea na masomo yao kama ilivyoelekezwa.

“Niwaagize uongozi wa Wilaya hususani Mkurugenzi ambaye najua hapa hayupo, watu wameambiwa wasisafirisafiri yeye anasafirisafiri, watu wasiende likizo yeye hayupo hapa, miundombinu haipo, sasa tutafika namna hii, nitakuja tena baada ya wiki mbili kuona hatua ambayo tumeifikia,” Alisema.

Wakati akitoa taarifa ya Wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Carolius Misungwi alieleza mikakati mbalimbali iliyowekwa na Wilaya ili kufanikisha azma ya serikali katika kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa madarasa hayo na wanafunzi hao kuendelea na masomo ifikapo mwezi Februari 2021.

“Wilaya imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari za Kalambo, Matai, Msanzi, Mwazye na Mambwe. Vyumba sita vya madarasa vya Shule ya Sekondari Wasichana matai vitatumika kwa muda wakati ujenzi wa vyumba 7 unakamilika katika shule ya Sekondari Matai,” Alisema.

Serikali kupitia miradi yake hiyo imetoa Shilingi 756,278,504.77/= kwaajili ya kujenga vyumba vya madarasa 18 wilayani Kalambo ambapo vyumba  15 ni vyashule ya Msingi na vyumba 3 vya Shule ya Sekondari Matai ambavyo havijakamilika na Kiasi cha Shilingi 229,678,504/= kwaajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 178 katika shule za msingi na Shilingi 6,600,000/= kwaajili ya ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika Shule za sekondari na kiasi cha Shilingi 160 kwaajili ya ujenzi wa Mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Matai ambayo nayo hayajakamilika na hivyo kufanya miundombinu yote kuwa katika silimia 42 ya utekelezaji wake.

 

No comments :

Post a Comment