Wednesday, December 30, 2020

MBUNGE MAKETE AKABIDHI SOLA ZAHANATI YA ILINDIWE-MANG'OTO





MBUNGE wa Makete Ndg Festo Sanga amekabidhi na kuzifunga Solar panel tatu ambazo aliahidi atawapatia wananchi wa Kijiji cha Ilindiwe kata ya Mang'oto endapo watamchagua alipopita kuomba kura wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu 2020.

Akikabidhi Solar hizo, Mbunge Festo Sanga amesema;

 "Nilipokuja kuomba kura mliniambia hitaji lenu la kwanza ni Umeme wa

Solar kwenye zahanati yenu hii, mlihitaji umeme kwasababu huduma nyingi zinakwama nyakati za usiku na hata zile zinazohitaji umeme. Zahanati hii inategemewa na sehemu kubwa ya wananchi wa Mang'oto, nimeona ni vyema nikaitekeleza mapema ili Mama zetu wanapohitaji huduma ya uzazi waipate masaa yote pakiwa na umeme, Lakini wahudumu wetu wapumzike kutumia tochi kuhudumia wananchi nyakati za usiku. Nawaomba mzitunze solar hizi ili zitusaidie kwa muda mrefu wakati tunahangaikia umeme wa REA". Amesema.

Baadhi ya Wananchi walioshuhudia utekelezaji wa ahadi hiyo wamesema, wameshangazwa na namna Mbunge alivyotekeleza ahadi hiyo kwa uharaka kwasababu ni ahadi ambayo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kwanza wa Mkoa wa Njombe na baadae viongozi wengine lakini haikutekelezeka, 

''huyu Sanga ametupa matumaini makubwa sanaaa sisi wananchi wa ilindiwe tunamuombea kwa Mungu ambariki kwa pale alipotoa kwaajili yetu.'' Amesema mmoja ya wananchi wa Ilindiwe.

No comments :

Post a Comment