Saturday, December 12, 2020

DKT.KALEMANI AWATAKA VIONGOZI WA TAASISI ZILIZOPO CHINI YA WIZARA YA NISHATI KUFANYA KAZI KWA KASI NA UFANISI

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati na menejimenti zake.( hawamo pichani)Kulia kwa Waziri Kalemani, ni Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato na kushoto kwa Waziri Kalemani ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Leonard Masanja.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akizungumza na Wakuu wa Taasisi na Menejimenti za Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati katika Kikao kazi cha Waziri wa Nishati na Wakuu wa Taasisi na Menejimenti za Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Leonard Masanja(aliyesimama) akimkaribisha Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nishati na Wakuu wa Taasisi na Menejimenti za Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati, Kikao kazi hicho kimefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF eneo la Makole, jijini Dodoma.

Washiriki wa kikao kazi cha Waziri wa Nishati na Wakuu wa Taasisi na Menejimenti za Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati, wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayumo pichani) wakati wa kikao kazi hicho kilichofanyika leo jijini Dodoma.

*************************************

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani,amewataka wakuu wa Taasisi zilipo chini ya Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa  wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa, kwa kasi kubwa, ufanisi na umakini ili kuhakikisha sekta ya Nishati inazidi kukua na kuimarika kwa maendeleo ya nchi na watu wake.

Waziri Kalemani ameyasema hayo Desemba 11,2020 wakati akiwa kwenye kikao na Wakuu wa

Taasisi na Menejimenti zake zilizopo chini ya Wizara ya Nishati, kilichofanyika katika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF eneo la Makole, jijini Dodoma

Katika kikao hicho, aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Stephen Byabato, Kaimu Katibu Mkuu Mhandishi Leornad Masanja, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Eward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi. Innocent luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zake.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kalemani, amewataka viongozi wa Taasisi hizo, kuhakikisha  kuwa miradi yote inayotekelezwa na Wizara hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora zaidi.

Aidha,Waziri Kalemani ameuelekeza uongozi wa TANESCO kuanzia sasa kuhakikisha hakuna mgawo wa umeme nchini na hakutokei ukataji wa umeme kabisa na pale wanapolazimika kukata umeme kutokana na sababu za msingi, taarifa itolewe kwa wananchi na warudishiwe umeme kama ilivyoahidiwa katika taarifa ya ukataji huo wa umeme.

Amesema, hii itawezesha uzalishaji viwandani pamoja na kuwezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote na hivyo kupelekea upatikanaji wa fedha zinazochangia katika ukuaji wa pato la Taifa linalotokana na Sekta ya Nishati na hivyo kuliletea Taifa maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Stephen Byabato, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika utendaji kazi, kufanya kazi kwa weledi na kujituma na amewaagiza Wataalam wa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuhakikisha taarifa za Wizara na Taasisi zake, zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati.

 

No comments :

Post a Comment