Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo wakati akikagua miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa ziara yake kwenye Shirika la Mawasiliano Tanzania, Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew na kushoto ni Mhandisi wa Shirika hilo, Marick Urassa
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo A. Mathew akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (anayesikiliza) alipotembelea Shirika hilo, Dar es Salaam.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba kuhusu mtambo wa zamani wa kupiga simu kwenye chumba cha makumbusho cha Shirika hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika hilo, Dar es Salaam
Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Nikusubila Maiko akifafanua jambo kwa Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kulia) wakati akikagua mitambo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa ziara yake kwenye Shirika hilo, Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew
Mhandisi wa Mtandao wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Amina Daudi akitoa maoni yake kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Faustine Ndugulile (hayupo pichani) wakati wa kikao na wafanyakazi alipotembelea Shirika hilo, Dar es Salaam
***********************************************
- Atoa onyo kwa kampuni zinazohujumu miundombinu ya TCCL
- Watakaoiba nyaya za shaba za TTCL kuhusishwa na uhujumu uchumi
Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amezipa siku 30 taasisi za umma zinazodaiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kulipa madeni kwa Shirika hilo ili liweze kujiendesha, kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma ya mawasiliano ya sauti na data kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi ili kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TTCL kwa lengo la kufahamiana na kuzungumza na wajumbe wa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew na Mejimenti ya Wizara hiyo
Ameongeza kuwa zaidi ya taasisi 20 za Serikali zinadaiwa na TTCL zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 30 ambapo zipo taasisi zinatumia huduma za mawasiliano za TTCL na zinakusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa mwezi ila hawako tayari kulipa huduma za TTCL
Vile vile, ametoa onyo kali kwa kampuni zinazohujumu miundombinu ya TTCL ili ishindwe kutoa huduma za mawasiliano kwa wateja wake kuwa waache tabia hiyo mara moja na wafanye biashara kwa misingi ya ushindani, vinginevyo Serikali itawachukulia hatua kali
Aidha, amesisitiza kuwa kwa watakaoiba nyaya za shaba za TTCL na kuuza kama chuma chakavu nao waache mara moja kwa kuwa watahusishwa na uhujumu uchumi kwa kudhoofisha utendaji kazi wa TTCL na kwa watakaobainika watachukuliwa hatua kali na Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama
Amewataka watendaji wa Wizara kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kufanya utafiti na tathmini ya kubaini mchango wa Sekta hii aidha wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja katika kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa kwa kuwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wanachi wanatumia huduma za mawasiliano ya data na sauti na kuendesha shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii kwa kutumia TEHAMA
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew amewataka watumishi wa TTCL kuwa wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na wajenge utaratibu wa kufuata na kuwahudumia wateja huko waliko badala ya kusubiri wateja kuwafuata ofisini
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kuwa amepokea maelekezo ya Waziri, Dkt. Ndugulile na ametoa rai kwa watumishi wote wa TTCL kujituma ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya mawasiliano yenye kasi ya brodibandi kutoka asilimia 49 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2025
No comments :
Post a Comment