Wednesday, December 30, 2020

DKT. GWAJIMA ATAKA UBORESHAJI WA HUDUMA ILI IWE CHACHU YA WANANCHI KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA


****************************************

Na Emmanuel Malegi-DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka

Hospitali za Rufaa za Mikoa nchi nzima kuhakikisha zinakarabati mashine mbalimbali za kutolea huduma ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi pindi wanapokosa huduma hizo pia ikiwa ni chachu kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima za afya ya NHIF na CHF iliyoboreshwa

Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo leo baada ya kutembelea vitengo mbalimbali vya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa za Mwananyamala na Amana zilizoko jijini Dar es Salaam na kubaini baadhi ya vifaa katika vitengo vya macho na meno kutofanya kazi pia kutokua na orodha ya huduma zinazotolewa.

“Nimeongea na watumishi ili kuwapa dira ya mwelekeo wa taifa letu katika kuwajibika ili kuweza kuwa na ufanisi katika kutoa huduma za afya ambapo hivi sasa tunaelekea kwenye bima ya afya kwa wote ya NHIF na CHF, ili wananchi wajiunge bila kusukumwa wanahitaji kuona huduma za afya zinaboreshwa na kupatikana”. Amesema Dkt. Gwajima.

Waziri huyo amesema ili kuweza kufanikisha azma ni kutembelea maeneo yanayotoa huduma ili kujionea hali halisi ambapo amegundua katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kitengo cha macho mashine ya kutengeneza miwani imeharibika toka mwaka 2017 na kupelekea wananchi wenye uhitaji kulazimika kutafuta huduma hiyo nje ya Hospitali.

Dkt. Gwajima ameonekana kushangazwa zaidi baada ya kugundua mashine hiyo inahitaji gharama ya Shilingi 18,000 tu kwa ajili ya kununua kifaa kilichoharibika na milioni moja za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kununua lenzi ili huduma za miwani ziweze kuendelea kutolewa.

Halikadhalika Dkt. Gwajima ametembelea kitengo cha meno na kupata taarifa ya kuharibika kwa kiti cha kutolea huduma hiyo ambacho hakijafanyiwa marekebisho kwa muda mrefu huku kiti kimoja tu ndicho kikifanya kazi hali inayopelekea kuwa na foleni ndefu ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Kufuatia hali hiyo Waziri Gwajima ameagiza kufanyika ukaguzi maalum wa pesa za Hospitali kuanzia mwezi Januari mpaka Disemba 2020 zimetumikaje mpaka zikashindwa kukarabati vifaa vya kutolea huduma hizo hospitalini hapo.

Ameongeza kuwa ripoti hiyo ikitoka italeta picha ya nini kilichokua kinafanyika huku lengo kubwa likiwa ni kuongeza ufanisi katika sekta ya afya na uzalishaji ili serikali inapowashawishi wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya basi kuwe na ushawishi wa kweli baada ya huduma kuimarishwa.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Hospitali zote nchini kutatua changamoto kama hizo ili siku akitembelea akute changamoto zote zimeshatatuliwa na wananchi wanapata huduma zote pasipo kulazimika kupata rufaa au kwenda kwenye vituo vya afya vya binafsi.

 

No comments :

Post a Comment