Tuesday, December 8, 2020

CCBRT WATEMBELEA MLOGANZILA, WAFURAHISHWA NA UTOAJI HUDUMA



HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila- imewekea mikakati mbalimbali ya

kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi ikiwemo huduma za kibingwa na kibobezi. 

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi wakati akizungumza na viongozi kutoka Hospitali ya CCBRT ambao wamefanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.

Dkt. Magandi amesema dhamira ya hospitali ni kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma bora za afya sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali za kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. 

Hospitali yetu ya Mloganzila inatoa huduma mbalimbali za afya ambapo kwa upande wa wagonjwa wa nje (OPD) kwa siku tunahudumia wagonjwa 400 hadi 490 na lengo ni kuhakikisha tunaendelea kuboresha huduma zetu.” amesema Dkt. Magandi.

Naye Meneja Uendeshaji kutoka Hospitali ya CCBRT Bw. Yohana Kasalawa amesema ziara yao ina lenga kupata uzoefu kutoka kwa wadau waliobobea katika  utoaji wa huduma za afya  pamoja na mambo mengine wameelezea kuridhishwa na utoaji wa huduma.

“CCBRT imepanua wigo wake wa kutoa huduma hivyo tumekuja kujifunza kwa wadau waliobobea kwanye masuala ya afya ili kupata ujuzi zaidi kutoka kwao” amesema Bw. Kasalawa.

“Tumetembelea hospitali mbalimbali na leo hii tumekuja hapa Mloganzila ambapo tumejifunza mengi hasa namna ambavyo tutaweza kuendesha huduma yetu mpya ya afya ya uzazi ambayo inatarajia kuanzishwa mapema mwezi wa nne mara baada ya jengo kukamilika” amesema Bw. Kasalawa.

Katika ziara hiyo ujumbe huo umetembelea maeneo mbalimbali ikiwemo huduma za uuguzi, rasilimali watu na utawala, huduma za ufundi, kliniki ya wagonjwa wa nje (OPD,)  idara ya uzazi na magonjwa ya wanawake na kitengo cha uhusiano.

 

No comments :

Post a Comment