***********************************************
Des 23
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
WAJUMBE wa kikao cha
bodi ya barabara mkoani Pwani ,wameazimia kuiomba Serikali kuangalia
namna ya kuunganisha wakala wa barabara (TANROADS ) na TARURA na kuwa
chini ya Wizara moja ili kuboresha huduma za mjini na vijijini ama
kuongeza mgawanyo wa fedha kwa TARURA kutoka asilimia 30 na kufikia
asilimia 40.
Mabadiliko hayo
yatasaidia TARURA kuongeza ufanisi wa kutatua changamoto ya ubovu wa
miundombinu ya barabara na kuboresha barabara hasa maeneo ya vijijini
ambapo wananchi wanapata kero zaidi.
Akizungumza wakati
akifunga kikao hicho,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo
alieleza, TARURA inapaswa ipewe nguvu kwa kuongezwa fedha za utekelezaji
kutoka asilimia 30 hadi 40 na TANROADS itoke kwenye asilimia 70 na kuwa
60 ili kuiongezea ufanisi TARURA.
“TANROADS inafanya kazi kubwa na TARURA inafanya kazi kubwa lakini kwasasa TARURA inahemewa na barabara nyingi za vijijini huku ikiwa na bajeti ndogo ya utekelezaji .
Aidha TARURA
inashindwa kupandisha hadhi baadhi ya barabara zake kwani ni lazima
ipige hodi kwa waziri mwenye dhamana anaeshughulika na TANROADS .
“Utekelezaji wake ni
mgumu kidogo ,wanakwama kiutendaji ,huku wananchi wa vijijini
wakiendelea kupata shida na wakibakia kuziba mashimo na kufanya
ukarabati zaidi kuliko kujenga barabara mpya kutokana na bajeti ndogo”
alieleza Ndikilo.
Mbunge wa jimbo la
Chalinze ,Ridhiwani Kikwete alisema ,jimbo la Chalinze ni miaka minne
mfululizo haijabahatika miradi inayotekelezwa kwa fedha za TARURA .
Kutokana na hilo
,mkuu wa mkoa Ndikilo alielekeza apelekewe taarifa ya ufafanuzi wa kila
halmashauri ,jumla ya miradi mipya na ya zamani ,mgawanyo wa fedha ili
kujiridhisha.
Mkuu wa wilaya ya
Mkuranga,Filberto Sanga aliomba Serikali kuangalia namna ya kuunganisha
wakala hizo ama kuiongezea fedha TARURA kwani kipindi kilichopita
wakulima wa korosho walishindwa kufikisha korosho zao barabarani
kutokana na barabara za vijijini kuwa mbovu .
Nae meneja wa
TANROADS Mkoani Pwani, Yudas Msangi alieleza bajeti ya mwaka wa fedha
2020/2021 ni bilioni 35.318 ambapo bilioni 24.297 ni ya matengenezo na
bilioni 11.021 ni ya miradi ya maendeleo.
Alifafanua pia
,tatizo walilonalo ni fedha kushindwa kusainiwa kwa wakati hivyo fedha
zinachelewa na kushindwa kutekeleza majukumu yao .
Hata hivyo
alibainisha,wananchi wanadai fidia ya bilioni 57 ,ambako wanatakiwa
wapishe ujenzi wa barabara mbalimbali katika mkoa huo.
Kwa upande wake
TARURA Mkoa bajeti ni bilioni 11.243 ambapo matengenezo ni bilioni
6.993, huku bilioni 2.95 miradi ya maendeleo na bilioni 1.3 miradi
maalum.
No comments :
Post a Comment