Na Shamimu Nyaki – WHUSM
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa
amesema kuwa lugha ya Kiswahili ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi hivyo ni lazima kuikuza na kuiendeleza ili ipate fursa nyingi katika soko la ndani na la kimataifa.Waziri Bashungwa ameyasema hayo Desemba 15, Jijini Dar es Salaam alipokua katika ziara ya kutembelea Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) akiwa pamoja na Naibu wake, Abdallah Ulega pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi ambapo amesema kwamba, watanzania wana wajibu wa kuipenda lugha ya Kiswahili na kuitangaza huku akisistiza kuwa ni jukumu la watanzania kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha.
“Naigiza BAKITA kuanzisha midahalo na mashindano ya uandishi wa insha za Kiswahili kuanzia shule za msingi na sekondari, lengo ni kuwafanya watoto wajue lugha hiyo kwa ufanisi na hatimaye taifa liwe na wabobezi katika lugha hiyo”,alisema Mhe. Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa Serikali itahakikisha nyaraka zote za kimahakama zinandikwa na kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili lengo ni kurahisiha mawasiliano ya watanzania katika kuzisoma na kuzielewa nyaraka hizo, huku akisisitiza kuwa mpango wa Serikali ni kukiongezea Kiswahili thamani katika ukanda wa Afrika na duniani.
Aidha, Bashungwa amesema kuwa Serikali itahakikisha sifa mojawapo ya wageni kufanya kazi nchini ni kujua lugha ya Kiswahili, lengo ni kukiuza Kiswahili pamoja na kukipa heshima kama utambulisho wa nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ulega amesema kuwa, Kiswahili ni bidhaa adhimu ambayo watanzania wanapaswa kujivunia nayo, huku akiwataka wabobezi wa lugha hiyo kutumia fursa zilizopo katika Ukanda wa nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki kufundisha lugha hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa, vifaa vya kisasa kwa ajili ya kujifunza ukalimani wa lugha vipo katika hatua ya mwisho ya manunuzi ambavyo upatikanaji wake utasaidia urahisi wa kujifunza ukalimani.
Vilevile, Kaimu Mtendaji Mkuu wa BAKITA Bi. Consolatha Mushi ameeleza kuwa Baraza hilo limepokea maombi kutoka nchi mbalimbali ambazo zimeonyesha nia ya kujifunza Kiswahili, ambapo pia limeandaa machapisho ambayo yatasambazwa katika nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
No comments :
Post a Comment