Wednesday, November 18, 2020

WIZARA YA MAJI YAANZA KUTEKELEZA ILANI YA CCM 2020-2025 KWA KISHINDO

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na Meneja wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini Tanzania, He Yifeng wakisaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa sh bilioni 70.5 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.

**************************************

Na Mohamed Saif, Mara

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji imeanza rasmi kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025.

Mhandisi Sanga alisema hayo Mkoani Mara Novemba 17, 2020 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Bilioni 70.5 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika maeneo ya Wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.

Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na Mkandarasi Kampuni ya UNIK Construction Company ya Lesotho.

“Tupo hapa kutekeleza Ilani ya Chama Tawala cha  CCM ya Mwaka 2020 hadi 2025 yenye kurasa 303 ambayo imetuelekeza kuhakikisha tunafikisha maji kwa wananchi wa Butiama na Musoma Vijijini kutoka Ziwa Victoria,” alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alimshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kupeleka fedha za kutekeleza mradi huo kama alivyokuwa ameahidi wakati wa Kampeni za uchaguzi Mkoani humo.

“Tunakila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Magufuli kwani mradi huu tunaosaini unatekelezwa kwa fedha za Serikali yake,” alisema Mhandisi Sanga.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Sanga alisema utajengwa kwa miezi 24 na kwamba kwa awamu ya kwanza utaweza kuzalisha kiasi cha lita milioni 17 dhidi ya mahitaji ya sasa ambayo ni lita milioni 12 kwa siku.

Aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi itaanza kunufaisha vijiji 19 yaani Wilaya za Butiama na Musoma Vijijini lakini pia kijiji kimoja kutoka Wilaya ya Bunda.

Alitaja maeneo yakayonufaika na mradi kuwa ni Miji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na vijiji vya Kwibara, Nyamisisye, Kiabakari, Singu, Mwanzaburiga, Kyawazaru, Kamugegi, Kyatungwe, Ryamugabo, Bumangi, Bisarye, Tiring’ati, Butiama, Rwamkoma, Buturu, Nyang’oma, Mayani, Katalyo na Tegeruka.

Mhandisi Sanga alibainisha kwamba eneo lenye mtandao wa majisafi litaongezeka kufikia asilimia mia moja kwa miji ya Mugango, Kiabakari na Butiama na kwamba zaidi ya wakazi 165,000 watapata huduma ya maji kwa asilimia mia moja.

Hata hivyo, Mhandisi Sanga alibainisha kwamba lengo ni kuhakikisha zaidi ya vijiji 39 kutoka kwenye wilaya hizo vinanufaika pindi mradi utakapokamilika kwa asilimia mia moja ambapo alisema kwa wakati huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni 35 kwa siku.  

Mradi unajengwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa wadau wa maendeleo Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa. Maendeleo wa Saudia (SFD)

Utiaji saini wa mradi huo mkubwa wa maji ni wa kwanza kutekelezwa tangu kuanza kwa  kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

 

No comments :

Post a Comment