Friday, November 13, 2020

RAIS MAGUFULI ASEMA UTUMBUAJI MAJIPU UTAENDELEA, AHAMISHA TIC KWENDA OFISI YA RAIS, AMUAHIDI MWINYI USHIRIKIANO


Charles James, Michuzi TV

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekihamisha Wizara kituo cha  Uwekezaji Tanzania (TIC)  kutoka Ofisi ya

Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais kwa lengo la kuongeza ufanisi na kazi zaidi.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma Rais Magufuli amesema amefanya maamuzi hayo ili kuongeza spidi na nguvu ya kuchochea wawekezaji nchini na hasa watanzania wenye nia ya kuwekeza kwenye nchi yao.

Akizungumzia sekta ya madini, Dkt. Magufuli amesema kwa hatua zinazochukuliwa na serikali sekta hiyo itaweza kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Amesema sekta nyingine ambayo serikali itatilia mkazo ni Utalii kwani imeajiri kundi kubwa la watu ambapo ajira zaidi ya Milioni nne zimetolewa.

" Tumejipanga kuongeza watalii kufikia Milioni tano, tutapanua wigo wa vivutio, kuimarisha utalii wa fukwe, kuongeza kasi ya utangazaji wa vivutio vyetu, lakini pia tutaendelea kupambana na ujangili ili kutunza vivutio vyetu." Amesema Dkt. Magufuli

Katika hotuba yake, Dkt Magufuli pia amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kuiongoza nchi hiyo huku akimuahidi ushirikiano katika kutekeleza ahadi zake alizozitoa kwa wanzanzibar wakati akiomba ridhaa ya kuliongoza taifa hilo.

" Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuleta maendeleo kwa pande zote mbili huku akisisitiza kutokua na mzaha kwa mtu yoyote atakayejaribu kuchezea amani na Muungano uliopo.

" Nitampa Dk. Mwinyi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza yale yote aliyoyaahidi kwa wanzanzibar lakini pia tutaendelea kusimamia utawala bora, kusimamia nidhamu kwa watumishi, kupambana na rushwa pamoja na kusimamia matumizi mazuri ya fedha za umma.

Kwa kifupi niseme utumbuaji wa majipu utaendelea, hatutoweza kumvumilia mtumishi yoyote mzembe lakini pia tutazingatia maslahi yao ili yaendane na maisha halisi ya watanzania hivyo watumishi wasiwe na wasiwasi na wachape kazi." Amesema Dkt.Magufuli.

 

No comments :

Post a Comment