Mkurugenzi wa
Uendelezaji Malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe
Rwiguza (kulia) akifafanua jambo mbele ya wataalam wa ukaguzi wa malisho
na rasilimali za vyakula vya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye
kiwanda cha kusindika chakula cha mifugo kinachojulikana kama “Musoma
Animal Feed” kilichopo mkoani Mwanza leo
Meneja wa Kiwanda cha
“Musoma Animal Feed” Bi. Maajabu Musa (mwenye kilemba cheusi) akitoa
maelekezo ya namna chakula cha mifugo kinavyotengenezwa kiwandani hapo
mbele ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wakaguzi
wa vyakula vya Mifugo kutoka Mikoa ya Mwanza, Arusha, Shinyanga na
Arusha wakati wa ziara yao waliyoifanya leo (13.11.2020) mkoani Mwanza.
……………………………………………………………………………….
Serikali imepiga
marufuku matumizi ya vyakula vilivyopoteza ubora wa kutumiwa na
binadamu na kutumiwa kama vyakula vya mifugo kabla ya kuthibitishwa
kwanza na wataalam wa maabara ya mifugo.
Hayo yamesemwa leo
(13.11.2020) na Mkurugenzi wa Uendelezaji Malisho na rasilimali za
vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha
mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya
Mwanza,Shinyanga, Singida na yaliyofanyika Mkoani Mwanza.
“Kumekuwa na mazoea
ya vyakula ambavyo vimeshapoteza ubora wa matumizi ya binadamu kutumika
kama vyakula vya mifugo hivyo ninapenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa
wafugaji, wazalishaji na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na
uzalishaji wa vyakula vya binadamu kuwa ni marufuku kutumia vyakula
hivyo bila Wizara yenye dhamana kuwa na taarifa na kujiridhisha kitaalam
kama chakula hicho kinafaa au la” Amesisitiza Dkt. Rwiguza.
Aidha Dkt. Rwiguza
amebainisha madhara yanayoweza kumpata mtu ambaye atatumia mazao ya
mfugo uliokula vyakula hivyo kuwa ni pamoja na kupatwa na magonjwa
mbalimbali kama vile Kansa.
Upande wake
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na rasilimali za
vyakula vya Mifugo Bw. Roggers Shengoto amesema kuwa mafunzo hayo
yamekuwa na manufaa makubwa kwa sababu sehemu zaidi ya asilimia 90 ya
wataalam walioalikwa walishiriki.
“Pia kupitia mafunzo
haya tumegundua kuwa bado kuna haja ya Halmashauri za vijiji kutenga
maeneo ya malisho ya mifugo na pia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya
mifugo bado hawazingatii sheria na kanuni za kufanya shughuli hizo
hivyo tuna imani wataalam hawa wataenda kuleta mabadiliko katika maeneo
yote yenye changamoto kwa mfugaji” Ameongeza Shengoto.
Nao baadhi ya
washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa wamenufaika na yote
waliyofundishwa ambapo wameahidi kuyafanyia kazi na kubadilisha utendaji
wao pindi wakirejea kwenye vituo vyao vya kazi.
“Kwa mfano, zamani
nilikuwa naenda kwa mdau kama Mkaguzi na nilikuwa natumia lugha ya
mamlaka lakini kupitia mafunzo haya nimefundishwa kumfuata mdau kama
rafiki na kuzungumza naye kwa lugha ya kawaida” Amesema mmoja wa
washiriki Veronica Ngoso.
Takribani wakaguzi
129 nchi nzima wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ili waweze kutekeleza
majukumu yao kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni.
No comments :
Post a Comment