Monday, November 9, 2020

Mfumuko wa bei Septemba wafanana na Oktoba, 2020

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2020 umebaki kuwa asilimia 3.1 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2020, anaripoti Doreen Aloyce.

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja ameyasema hayo leo Novemba 9,2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja akitoa takwimu za mfumuko wa bei za vitu mbalimbali kwa mwenzi Oktoba, mwaka huu,katika ofisi ya Takwimu jijini Dodoma leo Novemba 9,2020 mbele ya waandishi wa habari ambao hawapo pichani.(DIRAMAKINI).

Amesema, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2020 umekuwa sawa na mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2020 ambapo umechangiwa kupungua na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Oktoba,2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba,2019.

Minja amesema, baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Oktoba, 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba,2019 kuwa ni mchele kwa asilimia 4.2, mahindi kwa asilimia 12.4, unga wa mahindi kwa asilimia 3.2.

Pia kuna unga wa ngano kwa asilimia 0.9, unga wa mtama kwa asilimia 0.8, unga wa muhogo kwa asilimia 1.4, mihogo mibichi kwa asilimia 2.5, viazi vitamu kwa asilimia 5.4 na ndizi za kupikia kwa asilimia 6.3.

Minja amefafanua kuwa, kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Oktoba,2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba,2019 amesema, ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.2, gesi ya kupikia kwa asilimia 6.5, mkaa kwa asilimia 8.8, ukarabati wa vifaa vya usafiri kama magari kwa asilimia 8.3 na samani kwa asilimia 1.4 .

Wakati huo huo amesema hali ya mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2020 kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba 2020 umeongezeka hadi asilimia 4.84 kutoka asilimia 4.20 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2020.

Amesema, kwa upande wa Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba, 2020 umebaki kuwa asilimia 4.5 kama ilivyo kuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020.

 

No comments :

Post a Comment