Monday, November 16, 2020

MBUNGE WA ARUSHA MJINI MRISHO GAMBO APOKEA VIFAA VYA UJENZI KUTOKA KIWANDA CHA SUNFLAG KWA AJILI YA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI UNGA LIMITED

Mbunge wa wa Arusha mjini Ndg.Mrisho Mashaka Gambo akimshukuru Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Sun Flag jijini Arusha Bwn.Haroon Mhundi  baada ya kukabidhiwa Nondo zenye thamani ya shilingi Milioni 25 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule ya sekondari Unga limited.

  Na Jusline Marco-Arusha

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Ndg.Mrisho Gambo amepokea nondo zenye thamani ya shilingi

Milioni 25 kutoka  kwa wadau wa maendeleo katika kiwanda cha Sun Flag kilichopo jijini Arusha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Unga limited itakayoanza kujengwa hivi karibuni.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Unga limited,Gambo amesema mchakato wa ujenzi wa shule hiyo umetokana na wananchi hayo kuksbiliwa na adha ya muda mrefu upande wa shule ya sekondari.

Aidha amesema kuwa amesema kuwa katika uletaji wa maendeleo kwa wananchi hakupaswi kuwa na migogoro ya aina yoyote ile kwani kampeni zilisha pita na huu ni wakati wa utekelezaji wa maendeleo kwa wananchi.

Akikabidhi nondo hizo Bwn. Haroon Mhundi Meneja Mkuu kutoka katika kiwanda cha Sun Flag Mkoani humo amewapongeza wananchi wa jiji la Arusha kuwa na Mbunge mwenye uthubutu na kujali maslahi ya wananchi ambapo sifa hizo ndizo zilizosababisha uongozi wa kiwanda hicho kushirikiana naye katika uletaji wa maendeleo kwa wananchi wake.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa jiji la Arusha John Pima,Afisa elimu sekondari jiji la Arusha Mwalimu Valentino Makuka amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo ambao unatarajiwa kukamilishwa mwezi April mwakani utatoa fursa kwa wanafunzi wanaofaulu kupangiwa katika shule hiyo hivyo kupunguza misongamano ya wanafunzi kwenye shule nyingine.

Awali akizungumza katika hadhara hiyo Diwani wa kata hiyo Mahamod Said amesema kuwa umbali wa shule ambazo wanafunzi hupangiwa imekuwa ni chanzo cha wanafunzi wengi kukatisha masomo yao kutokana na wazazi wao kutokuwa na naili za kuwapa huku wengine wakipata mimba za utotoni.

Ameongeza kuwa katika Kata hiyo zipo shule mbili za msingi zenye watoto wasiopungua 3500 ambapo katika shule hizo kila mwaka wanafunzi 300 hadi 400 wanamaliza elimu ya msingi na kupangiwa shule za mbali kutoka na uhaba wa shule za sekondari katika eneo hilo.

Ameeleza kuwa hali hiyo hupelekea wanafunzi wasiopungua 10 hadi 30 wa kata ya Osunyai,Unga limited na Sokono 1 huacha shule kila mwaka kutokana na umbali wa shule za sekondari walizopangiwa,ukosefu wa nauli za kila siku pamoja na mimba za utotoni ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 na 2019 wanafunzi wasiopungua wawili walizikwa baada ya kubebwa na mafutiko ya mto wakijaribu kuvuka ili waweze kuwahi shuleni.

"Kila siku mzazi mwenye kipato cha shilingi elfu tano anatakiwa kumpa mtoto nauli ya shilingi elfu moja kila siku bado hajagawa kodi ya nyumba na matumizi,ukweli wanaumia"Alisisitiza diwani huyo

Naye mmoja wa wakazi wa kata hiyo Bi.Rukia Msengesi ametoa shukurani zake kwa diwani wa kata hiyo na Mbunge kwa hatua waliyoianza ya ujenzi wa shule hiyo kwani itakuwa mkombozi kwa wakazi wa kata hiyo kwani watoto wao wamekuwa wakiteseka katika suala la usafiri kutokana na shule kuwa umbali mrefu.

No comments :

Post a Comment