Mkurugenzi wa idara ya tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia ufunguzi wa kongamano hilo ambalo litakua la siku mbili
Washiriki wa Kongamano la pili la kitaifa la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza wakimsikiliza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi
Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha sayansi shiriki(MUHAS) Prof.Andrea Pembe akiongea kwenye kongamano hilo
Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki kongamano hilo ikiwa ni njia ya kujifunzaMganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi akiongea na wahiriki(hawapo pichani) kwenye kongamano la pili la kitaifa la sayansi la magonjwa yasiyoambukiza linalofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
**************************************
Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dar s salaam
Maisha ya watu yanafupishwa na magonjwa yasiyoambukiza kutokana na maradhi ya
Moyo,Kisukari,Saratani,Magonjwa ya njia ya hewa,Siko Seli,ajali, magonjwa ya figo,akili,dawa za kulevya na magonjwa sugu ya meno na macho.Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya wakati akifungua kongamano la pili la kitaifa la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza linalofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini hapa.
Prof. Makubi amesema kuwa magonjwa hayo yamesababisha hasara kubwa kwa taifa kwa maana ya kuondoa nguvu kazi na kurudisha nyuma maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla na hivyo kusababisha utegemezi sugu kwa familia na pia kuongeza mzigo mkubwa kwenye mfumo wa afya kwa kuwa ni magonjwa ya muda mrefu na yanatumia rasiliamali nyingi.
Akielezea hali ya magonjwa hayo Mganga Mkuu huyo alitaja takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa magonjwa hayo yamesababisha asilimia 33 ya vifo vyote nchini kwa mwaka 2017, ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
“Vifo hivi vimetokana zaidi na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwa asilimia 13, Kisukari 2%, Saratani 7% na ajali 11%, hali hii kwa ujumla haikubaliki na inatufanya tujumuike katika kujitathimini na kupanga mikakati ya pamoja ili kukabiliana na changamoto hii”.Alisisitiza Prof. Makubi.
Aidha, amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41 ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
Aliongeza kuwa Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya robo tatu (75%) ya vifo ambavyo kama ugonjwa ungetambulika mapema vingeweza kuepukika na huku mataifa ya uchumi wa kati na chini kama Tanzania yanaonekana kuathirika zaidi.
Hata hivyo Prof. Makubi aliwapongeza wanasayansi ambao wamewasilisha maandiko yao katika kongamano hilo ili kutoa ushahidi wa kisayansi wa ukubwa wa changamoto zilizopo katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na ushauri wa namna ya kuzitatua.
“Sote ni mashahidi, hali ilivyokua miaka kumi iliyopita sio ilivyo sasa,Serikali imeboresha miundo mbinu na kununua vifaa tiba na vifaa vya uchunguzi wa magonjwa ya kisasa vinavyowezesha wanasayansi kufanya kazi zao kiurahisi “. Alisema
Mganga Mkuu huyo alitoa wito kwa taasisi ,hospitali za taifa,kanda,Maalum na Mikoa kujiwekeza katika kutoa huduma kwa kasi pia kufanya tafiti za kisayansi zitakazowezesha wananchi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza zitakazowezesha kutoa mbinu mpya za matibabu.
Akitoa salamu za ukaribisho Prof. Andrea Pembe Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS) amesema jukumu mojawapo la chuo kikuu hicho ni kufanya tafiti mbalimbali ambazo zinalenga kutatua changamoto katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha za afya ya mtanzania.
Prof. Pembe aliahidi chuo chake kuendelea kufanya kazi bega kwa bega na Wizara ya afya katika juhudi za kuimarisha utoaji njia za kujikinga, kutibu na kupunguza matatizo yanayotokana na magonjwa yasioambukiza hapa nchini pamoja na matatizo mengine ya afya.
Naye, Prof. Appolinary Kamuhabwa, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kongamano hilo amesema katika kongamano hilo tafiti za kisayansi zaidi ya 200 zitawasilishwa kwa njia ya maongezi na kwa njia ya mabango na limehudhuriwa na wajumbe zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi.
No comments :
Post a Comment