Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani akizungumza katika uzinduzi huo kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya bima ya Sanlam Tanzania Khamis Suleiman wakati walipofafanua mambo mbalimbali kuhusu huduma hiyo kwenye hoteli ya Hyatt Regency mwishoni mwa wiki.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KATIKA kuendelea kuwajali wateja katika kutoa huduma zao benki ya
Standard Chartered kwa kushirikiana na kampuni ya Sanlam wamezindua huduma ya bima za bidhaa kwa wateja ili kuongeza thamani kwa wateja wao.Uzinduzi huo wa bidhaa za bima uliokwenda kwa kauli mbiu ya “Tunavilinda vyenye Tija,” umehusisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nyumba na magari kwa ulinzi na usalama wa mali za wateja wao.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani amesema kuwa suala la bima limekuwa na manufaa kwa sasa kutokana na ulinzi na usalama kupitia bima za bidhaa mbalimbali ikiwemo magari, nyumba na afya.
Amesema Tanzania ni sehemu salama na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Joseph Magufuli imekuwa ikishirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kujenga uchumi wa Taifa.
“Bima ina umuhimu mkubwa hasa katika ulinzi na usalama, watanzania lazima waelewe umuhimu wa kukata bima katika mabenki kwa manufaa yao binafsi na mali zao.”
Amesema kuwa huo ni ushirikiano wa kibiashara kwa maendeleo ya jamii na taifa la Tanzania na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kuendeleza bima zikiwemo za sekta ya madini na afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sanlam Tanzania Khamis Suleiman mabenki kuanza kuuza bima ni muhimu kwa kuwa wanafahamu ni nini mteja anacho na anachoweza kununua.
Amesema kuwa Kampuni hiyo iliyotimiza miaka 102 tangu kuanzishwa kwake ina malengo ya kufikia asilimia 50 ya watanzania wanaomiliki bima hadi kufikia mwaka 2030, na bima hizo zikiwa ni pamoja na bima za nyumba na magari.
Vilevile amesema, Sanlam imekuwa nchini kwa miaka 20, wakiwa katika nchi 44 zikiwemo nchi zote za Afrika Mashariki na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa ustawi wa jamii na taifa la Tanzania.
Amesema kuwa watanzania wachukue bidhaa za bima kutoka Standard Chartered kwa kuwa wanavilinda vyenye tija.
No comments :
Post a Comment