Meneja Wa Kanda Crdb Bw.Lusingi Sita Akitoa Neno La Ufunguzi Katika Jukwaa La Kongamano La Wanawake Jijini Mwanza
Mkuu
Wa Mkoa Wa Mwanza Bw. John Mongella Akihutubia Washiriki Kwa Ajili Ya
Ufunguzi Wa Jukwaa La Kongamano Maalum La Wanawake Liliandaliwa Na Benk
Ya Crdb Jijini Mwanza
======= ======== ========
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza awataka wanawake kuchangamkia fursa za CRDB Malkia
Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa
kongamano la uwezeshaji wanawake mkoa wa Mwanza ili kuonyesha fursa
mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kwa wanawake. Akifungua kongamano
hilo Mongela ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa kongamano hilo huku
akiwataka wanawake kuchangamkia fursa zinazotolewa na benki hiyo kupitia
CRDB Malkia.
Mongela aliipongeza Benki ya CRDB kwa hatua ambayo
imechukua hivi karibuni ya kupunguza riba ya mikopo inayotolewa kwa
wanawake wajasiriamali kutoka asilimia 24 hadi asilimia 14. Akitoa
hotuba yake katika kongamano hilo lililohudhuriwa na wanawake
wajasiriamali zaidi ya 300, Mongela alisema hatua ya Benki ya CRDB
kupunguza riba kwa kutoka asilimia 24 iliyokuwa ikitozwa mwanzo hadi
asilimia 14 itasaidia wanawake wengi zaidi kuchangamkia fursa ya mikopo
hiyo.
“Kupungua kwa riba ina maana inapunguza mzigo mkubwa wa
marejesho kwa wanawake na kuwafanya kuwa na fedha nyingi kwa ajili ya
uwekezaji katika biashara zao na hivyo kupelekea kufanikisha zaidi,”
alisema Mongela.
Mongela alisema pamoja na tafiti kuonyesha
wanawake wamekuwa na ushiriki mkubwa katika shughuli za uchumi nchini,
kwa asilimia 54, ni asilimia 60% tu ya wanawake ndio wenye kufikiwa na
huduma rasmi za kifedha.
“Niwapongeze pia kwa kuboresha masharti
ya dhamana ili kutoa fursa kwa wanawake wengi zaidi kuweza mikopo,”
aliongezea Mongela huku akiwataka wanawake pia wajitokeze kwa wingi
kufungua akaunti ya Malkia itakayosaidia kufanikisha malengo yao kwa
kujiwekea akiba kidogokidogo jambo litakalosaidia kujenga imani kwa
taasisi za fedha.
Mongela alisema jitihada hizo zinazofanywa na
Benki ya CRDB katika uwezeshaji wa makundi mbalimbali ya wananchi
zimekuwa na msaada mkubwa katika kuisaidia Tanzania kufikia lengo la
kuwa nchi yenye uchumi wa kati.
“Azma ya Serikali ni kuendelea
kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara kwa wanawake ili kuwawezesha
kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika
jamii,” alisema Mongela.
Naye Mbunge wa Ilemela, Mheshimiwa
Angelina Mabula aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma ya Malkia
Rafiki katika matawi yake akisema kuwa huduma hiyo itasaidia kwa kiasi
kikubwa kotoa elimu ya fedha kwa wanawake na usaidizi wa kutosha katika
huduma ya CRDB Malkia. Benki ya CRDB imeweka wataalamu wa uwezeshaji
wanawake wajulikanao kama “Malkia Rafiki” katika mtandao wa matawi yake
yote nchi nzima.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya CRDB, Mkurugenzi wa Manunuzi wa Benki ya CRDB, Pendason
Philemon alisema huduma ya CRDB Malkia imelenga katika kumtambua, kumpa
nafasi na kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kufikia malengo yake
kupitia mikopo ya biashara na ujasiriamali, kujiwekea akiba kwa akaunti
ya Malkia na mafunzo ya uendeshaji biashara.
“Mpaka kufikia
mwishoni mwa mwezi June mwaka huu, Benki yetu tayari ilikuwa imekwisha
toa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 600 kwa wanawake zaidi ya
elfu 55,” alisema Pendason huku akibainisha kuwa zaidi ya wanawake
30,000 tayari wameshajiunga na akaunti ya Malkia.
Mkuu
Wa Mkoa Wa Mwanza Watano Kutoka Kulia Akiwa Katika Picha Ya Pamoja Na
Viongozi Wa Benki Ya Crdb Na Baadhi Ya Washiriki Mara Baada Ya Kufungua
Jukwaa La Kongamano Maalum La Wanawake Jijini Mwanza
Pendason
alisema pamoja na mafanikio ambayo Benki ya CRDB imeyapata katika
kumuwezesha mwanamke, bado idadi ndogo ya wanawake wamekuwa wakijitokeza
kupata huduma kutokana na changamoto ya riba, masharti magumu ya
dhamana na kukosa uelewa wa huduma za kifedha.
“Tukiwa Benki ya
kizalendo inayothamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa
letu, tukasema ni vyema tukatafuta suluhisho la changamoto hizi ili
kuweza kumsaidia mwanamke kufankisha malengo yake zaidi.
Baadhi
Ya Washiriki Ambao Wamejitokeza Katika Jukwaa La Kongamano Maalum La
Wanawake Lililoandaliwa Na Benki Ya Crdb Jijini Mwanza
Pendason
alisema CRDB Malkia sasa hivi inawawezesha wanawake kupata mikopo kwa
riba ndogo ya asilimia 14 kulinganisha na asilimia 24 iliyokuwa ikitozwa
mwanzo huku masharti ya upatikanaji wa mikopo yakirahisishwa kwa kiasi
kikubwa.
“Kupungua kwa riba kuna maana wanawake sasa wanaweza
kukopa zaidi na kwa gharama nafuu kulinganisha na mwanzo hivyo kusaidia
kufanikisha malengo yao kwa uharaka zaidi,” alisema Pendason.
Akihitimisha
kongamano hilo, Pendason alisema, Benki ya CRDB imejipanga vilivyo
kushiriki katika safari ya mafanikio ya wanawake wote wa Tanzania na
kuwaomba wanawake wajitokeze kwa wingi katika matawi ya Benki ya CRDB
ili kuanza kufurahia huduma hiyo mpya ya CRDB Malkia. “Ukifika tawini
ulizia Malkia Rafiki naye atakusaidia kuanza safari yako ya mafanikio,”
alihitimisha Pendason.
No comments :
Post a Comment