………………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI
BENKI ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) imekikabidhi kikundi cha wakulima wa mboga mboga
cha wanawake cha Faraja Women Group hundi ya shilingi milioni nne kwa
ajili ya kununua mashine ya kumwagilia ili kuwa na kilimo cha faida na
siyo cha kujikimu.
Akikabidhi hundi hiyo
kwa kikundi hicho ambacho kiko ndani ya Chama Cha Ushirika wa
Umwagiliaji Cha Ruvu (CHAURU) kilichopo Halmashauri ya Chalinze wilayani
Bagamoyo mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa
mashine hiyo itawafanya wanachama hao kuwa na kilimo cha uhakika.
Ndikilo alisema kuwa
ili wakulima hao wa mboga mboga kuwa na kilimo cha faida na siyo cha
kujikimu kwani mbali ya kufanya biashara pia wataweza kutumia kilimo
hicho kama lishe kwa familia na ziada watauza.
“Wanawake ndiyo
wakulima wakuu ikilinganishwa na wanaume hivyo wana nafasi kubwa ya
kuinua uchumi wa familia na Taifa kupitia kilimo hivyo lazima waungwe
mkono kwa hali na mali,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa licha ya
wanawake kuwa ndiyo wengi wanaojishughulisha na shughuli za kilimo
lakini bado wanakabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na kutomiliki
ardhi, miundombinu duni na kutoshirikishwa kwenye matumizi ya fedha
zinazopatikana kwenye shughuli hizo.
“Tunapaswa kuunga
mkono juhudi hizo za wanawake kwa kuwasaidia kwa hali na mali ili kuweza
kuwaondolea changamoto zinazowakabili ili zisiwe kikwazo kwao katika
sula zima la kilimo ambacho ni mkombozi wao na familia zao,” alisema
Ndikilo.
Kwa upandewake
mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo Rosebud Kurwijila
alisema kuwa wameamua kuwapatia hundi hiyo ili iwasaidie katika harakati
zao za kilimo hicho cha mbogamboga ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kurwijila alisema
kuwa benki yao imeona iunge mkono serikali kuyawezesha makundi
mbalimbali ili yaweze kujikwamua na kuongeza kipato kwa kuwapunguzia
changamoto zinazowakabili ikiwemo hiyo ya vifaa kwa ajili ya
umwagiliaji.
Naye mwenyekiti wa
kikundi hicho Salma Mponda alisema kuwa wanashukuru kwa msaada huo ila
wanaomba kupatiwa mafunzo kwa ajili ya ukopaji na utunzaji wa fedha ili
waweze kufikia kuwa wakopaji wakubwa toka wakopaji wadogo.
Mponda alisema kuwa
walianzisha kikundi hicho cha mbogamboga baada ya kuona kuwa mara
wamalizapo shughuli zao za kilimo cha mpunga hawana jambo la kufanya na
kuomba eneo kwa ajili ya kulima mbogamboga na kikundi hicho kilianzishwa
mwaka 2016 na kupatiwa usajili na kwa sasa kina wanachama25.
No comments :
Post a Comment