Friday, October 9, 2020

WACHIMBAJI WA TANZANITE WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA MASOKO

Wadau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye mkutano wa kujadili uwekezaji
katika maadhimisho ya wiki ya uwekezaji duniani.
Mkurugenzi mtendaji wa Alpha Associates Ltd, Dk Alfonce Massaga
akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara


Wadau wa madini wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali
wa uwezeshwaji waliokuwa wakitoa elimu ya uwekezaji.
 

Na Mwandishi wetu, Mirerani

KATIKA kusherehekea maadhimisho ya wiki ya uwekezaji duniani,
wachimbaji madini ya Tanzanite mji mdogo wa Wilaya Simanjiro Mkoani
Manyara, wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana kwenye masoko ya
mitaji na dhamana ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.

Mkurugenzi mtendaji wa ya Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana,
Nicodemus Mkama ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite, na kusema wachimbaji hao wanaweza kuwekeza kwenye hati fungani za Serikali, hisa na hati fungani za kampuni katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Amesema wachimbaji hao wanaweza kuunda kampuni kupitia umoja wao na
kuweza kupata mitaji itakayotumika kununua vifaa vya uchimbaji.

"Tutaendelea kufanya mawasiliano na wadau hawa wa madini ili fursa
zinapotokea wachimbaji waweze kunufaika nazo," amesema Mkama.

Mwenyekiti wa kamati ya Tanzanite, Yusuf Money amesema hivi sasa
uchimbaji wa madini ni mgumu hivyo wadau hao wanapaswa kuungana na
kuwa na umoja.

Amesema hawatapata mjomba au mtu wa kuwasaidia zaidi ya kuungana na
kuwa na umoja wa wachimbaji kwa lengo la kuungana.

Pia Mkurugenzi mtendaji wa Alpha Associate Ltd, Dkt. Alfonce Massaga amesema wachimbaji wanapaswa kujitambua kwani wanamiliki leseni ambayo ni mtaji mkubwa.

Katibu wa chama cha wachimbaji mkoani Manyara (Marema) Tawi la
Mirerani, Rachel Njau ameishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo
kwani yamewajengea uwezo katika suala zima la uwekezaji.

Njau amesema ili kuunga mkono mafunzo hayo wachimbaji 100 au 50
watajiunga kwa umoja ili kufanikisha mpango wa kuwa pamoja na
kuanzisha umoja.

Mchimbaji Zephania Joseph amesema elimu ya wachimbaji wengi wa madini
ni ndogo hivyo wanapaswa kuelimishwa mara kwa mara juu ya uwekezaji
huo.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni wiki ya uwekezaji ni "Kuongeza Uelewa
na kulinda Maslahi ya Uwekezaji"

 

No comments :

Post a Comment