Thursday, October 8, 2020

WACHIMBAJI TANZANITE WATAKIWA KUTUMIA FURSA YA MASOKO


Mkurugenzi mtendaji wa Alpha Associates Ltd, Dk Alfonce Massaga akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Wadau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye mkutano wa kujadili uwekezaji katika maadhimisho ya wiki ya uwekezaji duniani.
Wadau wa madini wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa uwezeshwaji waliokuwa wakitoa elimu ya uwekezaji.
………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Mirerani
KATIKA kusherehekea maadhimisho ya wiki ya uwekezaji duniani, wachimbaji madini ya Tanzanite mji mdogo wa Wilaya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji na dhamana ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao. 
Mkurugenzi mtendaji wa ya Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana, Nicodemus Mkama ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite.
Amesema wachimbaji hao wanaweza kuwekeza kwenye hati fungani za serikali, hisa na hati fungani za kampuni katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
Amesema wachimbaji hao wanaweza kuunda kampuni kupitia umoja wao na kuweza kupata mitaji itakayotumika kununua vifaa vya uchimbaji. 
“Tutaendelea kufanya mawasiliano na wadau hawa wa madini ili fursa zinapotokea wachimbaji waweze kunufaika nazo,” amesema Mkama. 
Mwenyekiti wa kamati ya Tanzanite, Yusuf Money amesema hivi sasa uchimbaji wa madini ni mgumu hivyo wadau hao wanapaswa kuungana na kuwa na umoja.
Amesema hawatapata mjomba au mtu wa kuwasaidia zaidi ya kuungana na kuwa na umoja wa wachimbaji kwa lengo la kuungana.
Mkurugenzi mtendaji wa Alpha Associate Ltd, Dk Alfonce Massaga amesema wachimbaji wanapaswa kujitambua kwani wanamiliki leseni ambayo ni mtaji mkubwa.
Katibu wa chama cha wachimbaji mkoani Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Rachel Njau ameishukuru serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani yamewajengea uwezo katika suala zima la uwekezaji.
Njau amesema ili kuunga mkono mafunzo hayo wachimbaji 100 au 50 watajiunga kwa umoja ili kufanikisha mpango wa kuwa pamoja na kuanzisha umoja.
Mchimbaji Zephania Joseph amesema elimu ya wachimbaji wengi wa madini ni ndogo hivyo wanapaswa kuelimishwa mara kwa mara juu ya uwekezaji huo.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni wiki ya uwekezaji ni kuongeza uelewa na kulinda maslahi ya uwekezaj.

No comments :

Post a Comment