Monday, October 5, 2020

TAARIFA ZINAZOCHAPISHWA KWENYE GAZETI LA SERIKALI ZINATUMIKA KUTATUA MIGOGORO NA KUFANYA MAAMUZI YA KISHERIA


 Na. James Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 5 Oktoba, 2020.

Gazeti la Serikali lilianzishwa kwa lengo la kuchapisha na kuhifadhi taarifa muhimu zinazotumika kama marejeo katika kutatua migogoro mbalimbali na kufanya maamuzi muhimu yakiwemo ya kisheria.

Msaidizi wa Maktaba Mwandamizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Beatrice Mganga ameainisha baadhi ya migogoro inayotatuliwa kupitia Gazeti la Serikali kuwa, ni ya umiliki wa ardhi, mirathi na mali isiyo na mwenyewe.

Akizungumzia lengo la uanzishwaji wa gazeti hilo, amesema, matangazo ya Gazeti la Serikali huwa rasmi kiutendaji na kwa utekelezaji wa majukumu mbalimbali hapa nchini.

Naye, Mkutubi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Halima Rauna amefafanua kuwa, Gazeti la Serikali ni kielelezo muhimu cha taarifa za Serikali, taasisi binafsi, wananchi na wadau mbalimbali zinazotumika katika utendaji wa kila siku.

Gazeti la Serikali lilianzishwa kwa mujibu wa “General Orders” kifungu C.56- C.62 ya mwaka 1957, pamoja na marekebisho yake kwenye Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma Kifungu C.28-C.30 toleo la mwaka 1971, kifungu C.28-C.31 toleo la mwaka 1994 na Kifungu C.27-C.30 toleo la mwaka 2009.

Kutokana na umuhimu wa Gazeti hili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, inazihimiza Taasisi za Umma na wananchi kuwasilisha taarifa zinazopaswa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali ili ziweze kutumika kutatua migogoro katika jamii na kuiwezesha Mahakama kufanya maamuzi ya kisheria.

 

No comments :

Post a Comment