Monday, October 12, 2020

PROF.SHEMDOE:WAWEKEZAJI MJE MUWEKEZE MKOA WA TANGA YAPO MAENEO MENGI YA VIWANDA

Shemdoe alisema kuwa Tanzania inawezesha zaidi  katika uwekezaji na maeneo mengi ya uwekezaji yapo na yanatekelezwa kwa ajili yao hivyo kuwataka wawekezaji wanaohitaji waje kuwekeza ili walipe kodi, walete ajira na mambo mengine yanaendana na uwekezaji.
…………………………………………………………………………….

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

KATIBU Mkuu wizara ya viwanda na biashara Prof. Riziki Shemdoe ametoa wito kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchi waje katika mkoa wa Tanga kwani yapo maeneo mengi ya kuwekeza katika sekta viwanda.

Wito huo aliutoa jana alipotembelea kiwanda cha Nellkanth Chemical L.t.d kilichopo eneo la Amboni jijini Tanga  wakati alipofanya ziara ya siku moja kutembelea viwanda mkoani hapa.

Shemdoe alisema kuwa Tanzania inawezesha zaidi  katika uwekezaji na maeneo mengi ya uwekezaji yapo na yanatekelezwa kwa ajili yao hivyo kuwataka wawekezaji wanaohitaji waje kuwekeza ili walipe kodi, walete ajira na mambo mengine yanaendana na uwekezaji.

“Wito wangu kwa wawekezaji wengine waje wawekeze Tanzania, waje wawekeze mkoa wa Tanga kuna maeneo mengi sana na magodauni sana ambayo yapo kwa sasa na yangeweza kutumika kwa ajili ya viwanda, waje wakijua hapa nchini tuna blue print ambayo inatekelezwa kwa ajili ya wawekezaji ili waje walipe kodi na kuleta ajira kwa wananchi wetu” alisema.

Aidha alizungumzia suala la uzalishaji katika kiwanda hicho na kusema kuwa kiwanda hicho kina maeneo makubwa yanayofaa kuwekeza biashara zaidi ya uzalishaji uliopo wa chokaa kwani wana maeneo mengine zaidi ya ekari 2500 ambayo wanaanzisha kulima chumvi ambayo imeshaanza kuonekana.

“Eneo hili zamani lilikuwa halilimiki hapa lakini sasa kuna migodi ambayo inatoa madini ambayo inazalishwa na kuleta faida nchini kwani wanalipakodi na kusaidia wananchi kupata ajira, na vilevile kuanzishwa kwa shamba hili kutatufanya sisi kuacha kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi” alibainisha.

Hata hivyo alisema kuwa kiwanda hicho kimefanya kazi kubwa kutokana na uzalishaji wake kwani wameajiri wananchi zaidi ya 2000 ambao wako kiwandani hapo na wengine takribani 4000 wako kwenye maeneo mengine ambayo yanamilikiwa na mwekezaji huyo.

Naye Mkurugenzi mzalendo wa kiwanda hicho Rashid Amour (Liemba) alisema kuwa kupitia uzalishaji mkubwa wa kiwanda hicho tayari wameshateka masoko katika nchi mbalimbali za Afrika mashariki na Maziwa makuu ambapo wamekuwa wakipeleka bidhaa zao katika masoko ya ushindani.

“Kwakweli mpaka sasa hivi soko letu kubwa liko Congo, lakini siyo Congo pekeyake bali tumeziteka nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda, kwa sasa hivi bidhaa yetu tunashukuru tumezishika nchi zote za Afrika mashariki maana wao ndiyo wanapambana na sisi” alifafanua Liemba.

“Kama mnavyofahamu biashara ni ushindani na sisi tumeingia kwenye ushindani nan chi hizi, tunaiomba serikali iweze kutusaidia katika ushindani huu na kama itatusaidia nina hakika ushindani huu tutaushinda bila matatizo” aliongeza.

Aidha alieleza kwamba kwa sasa ushindani mkubwa wanaoupata ni kutoka nchi ya Afrika kusini ambako pia alizungumzia hofu yake kuhusu soko hilo kwamba nchi ya Congo imeshaingiliwa na nchi ya China ambayo inatengeneza bidhaa hiyo ya chokaa kupeleka huko.

“Kwa sasa hivi ushindani wetu mkubwa uko South Africa kwa Congo, sasa hivi Congo wameingia wachina, wachina wanajitahidi sana kutengeneza bidhaa kuleta hapa nao ni chokaa kama sisi  na mpaka sasa hivi tunajitahidi kupambana nao” aliongeza.

Hata hivyo alibainisha kwamba kiwanda hicho kinapambana katika soko la chokaa lakini zipo biashara nyingine wanazozalisha kama vile magnissium (MGO) ambavyo vyote vinatumika kusafishia cooper ambapo pia alitoa takwimu ya bidhaa wanazosafirisha kupeleka kwenye masoko nje ya nchi.

“Congo peke yake tunapeleka siyo chini ya tani elfu kumi lakini kipindi cha nyumba tulikuwa tunakwenda mpaka tani elfu ishirini, Kenya na Zambia nako pia tunapeleka tani kumi vilevile kwahiyo ni tani elfu ishirini kwa mwezi” alifafanua.

 

No comments :

Post a Comment