Friday, October 9, 2020

OMBI LA JPM KWA WATANZANIA BAADA YA KUPOKEA SIMU YA KENYATTA KUHUSU CORONA



Na Said Mwishehe, Michuzi TV

RAIS Dkt. John Magufuli amewaomba Watanzania kushirikiana na wananchi wa Kenya katika kufanya maombi ya siku tatu kuanzia leo kwa ajili ya
kumuomba Mungu ili nchi hiyo iondokane na gonjwa la Corona ambalo
limeendelea kuzitesa nchi mbalimbali duniani ikiwemo nchi hiyo.

Akizungumza leo Oktoba 9, 2020 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano
wake wa kuomba ridhaa ya watanzania ili wamchague tena katika Uchaguzi
Mkuu mwaka huu, Dkt.Magufuli amesema miezi kadhaa iliyopita Tanzania
pamoja na nchi nyingine zilikuwa zinasumbuliwa na Corona.

Amesema kuwa, Tanzania walikaa pamoja chini ya uongozi wa
viongozi wa dini na kisha kumuomba Mungu ili aepushe  gonjwa hilo la
Corona na katika Mungu hakuna linaloshindikana.

"Ugonjwa wa Corona Tanzania umeondoka. Leo asubuhi nilikuwa naongea na
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta naye ameamua  katika kipindi cha siku
tatu kuanzia leo Ijumaa, kesho Jumamosi na Jumapili kumuomba Mungu ili
ugonjwa wa Corona uondoke Kenya.

"Tushirikiane na Wakenya ili ugonjwa wa Corona Kenya uondoke kama
ambavyo Mungu ameuondoa Tanzania, tuna hakika Mungu wetu atatusikia na
gonjwa hilo litaondoka Kenya, Mungu ukimuomba hakuna
kinachoshindikana.

Kwa kukumbusha tu wakati wa janga la Corona likiwa limeshika kasi Rais
Magufuli pamoja na kuwaomba watanzania kuchukua tahadhari zote kama
sehemu ya kukabiliana na ugonjwa huo alitumia nafasi yake kuwaomba
watanzania kwa umoja wao kufanya maombi ya siku tatu kwa ajili ya
kumuomba Mungu kuwapusha na janga hilo, maombi ambayo Mungu amejibu na leo hii Tanzania hakuna Corona.

No comments :

Post a Comment