Friday, October 9, 2020

DKT. MAGUFULI AFICHUA SIRI YA UMUHIMU WA JIJI LA DAR



*Aeleza namna linavyochangia pato la Taifa.

Na Said Mwishehe, Mchuzi TV

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi(CCM) Dkt.John Magufuli amefichua siri ya umuhimu wa Jiji
la Dar es Salaam ambalo idadi ya watu kwa sasa imefikia milioni sita.

Dkt. Magufuli ametoa siri hiyo leo mbele ya maelfu ya wananchi wa Jiji
la Dar es Salaam ambao wamejitokeza kwenye mkutano wake wa kampeni za
kuomba ridhaa kwa Watanzania ili achaguliwe tena kuongoza nchi kwa
kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza
umuhimu wa Jiji hilo katika kuleta maendeleo ya nchi.

Amefafanua kuwa Jiji la Dar es Salaam ni muhimu sana  nchini kwani
ndilo Jiji lenye idadi kubwa ya watu kuliko maeneo yote nchini
Tanzania.
"Kwa sasa Dar es Salaam kuna watu milioni sita na ifikapo
mwaka 2030 litakuwa na watu milioni 10 na hivyo kulifanya kuwa
miongoni mwa majiji manne makubwa na yenye watu wengi barani Afrika". Ameeleza.

Ameongeza mbali ya kuwa na idadi kubwa ya watu, Jiji la Dar es Salaam
ni lango kuu la biashara nchini kwani linatoa mchango mkubwa
katika kuchangia pato la Taifa na maendeleo kwa ujumla na limekuwa
likiongoza kwa uchangiaji mapato na hasa mapato ya kodi kwa asilimia
90.

Dkt. Magufuli ametumia nafasi hiyo kutoa takwimu za mapato tangu mwaka
2015 hadi mwaka 2020 ambapo kwa mwaka 2016/2017
ilichangia Sh.trilioni 12.6 sawa na asilimia 88.6 na mwaka 2017/2018
ilichangia Sh.trilioni 13.6 sawa na asilimia 89.

Amesema mwaka 2018/2019 Jiji la Dar es Salaam lilichangia mapato ya
Sh.trilioni 13.9 sawa na silimia 88.7 na mwaka 2019/2020 limechangia
Sh.trilioni 16.6 ambayo ni sawa na asilimia 89. 7. Na kwa kipindi cha
miaka mitano Jiji la Dar es Salaam limeendelea kuongoza katika pato la
Taifa.

"Ndugu zangu wana Dar es Salaam, hili ni lango kuu
la uchukuzi na lango la usafirishaji, sio hapa tu nchini bali na nchi
nyingine zinazotuzunguka, nchi yetu inapakana  na nchi nane kati ya hizo
nchi sita hazina bandari.Kwa kuzingatia hayo yote nilipokuja kuomba
kura niliahidi mambo mengi lakini nitataja manne."amesema Dkt.Magufuli
wakati anazungumzia umuhimu wa Jiji hilo.

Amefafanua mwaka 2015 wakati anaomba ridha aliahidi kuimarisha ulinzi
na usalama, kuimarisha miundombonu mbalimbali, kuboresha huduma za
jamii ikiwemo afya, elimu maji na umeme pamoja na ahadi ya nne ilikuwa
ni kuboresha mazingira ya biashara kwa ajili ya wananchi wa Jiji la
Dar es Salaam na Watanzania wote.

"Nashukuru kwa miaka mitano tumeweza kutekeleza ahadi hizo kwa
vitendo, wagombea udiwani na wabunge wamekuwa wakieleza mambo ambayo yametekelezwa.

Wakati tunaingia Dar es Salaam kulikuwa na vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha.

"Waliokuwa wanakwenda benki hawakuwa na uhakika wa fedha zao kufika
salama, hali hiyo imedhibitiwa na sio Dar es Salaam tu bali hata
maeneo ya nje ya Jiji hilo yakiwemo ya Kibiti na Mkuranga ambako
waliokuwa wanafanya vitendo hivyo Dar wanakwenda kujificha
huko,"amesema.

Kuhusu ahadi ya miundombinu, Dkt.Magufuli amesema wagombea ubunge
wameeleza mambo mengi yamefanyika, barabara za lami zimejengwa katika
mitaa ya Dar es Salaam  na ukijumlisha barabara za lami ni zaidi ya
kilometa 2000 zimejengwa ambapo kiasi cha Sh.bilioni 660 zimetumika.

Pia amesema barabara nyingine bado zinaendelea kujengwa na fedha
tayari zipo kufanikisha ujenzi huo huku akiamua kumjibu mmoja ya
wagombea urais ambaye amekuwa akieleza barabara ya kutoka Kimara hadi
Kibaha ni pana sana.

"Kwanza sio kweli kule Hoston nchini Marekani kuna
barabara ina njia 26 lakini hata kama kwa mfano ingekuwa ni barabara
yetu ni pana hakuna ubaya." Amesema.

"Sio lazima ili kitu kizuri basi kiwepo Ulaya tu, mbona Mungu aliamua
kutupa mtu wa kwanza hapa Tanzania, hakushangaa kitu, mbona tunao
mlima mrefu hapa kwetu lakini wala hakushangaa, mbona madini ya
Tanzanite yapo Tanzania tu na hata mti mrefu kuliko yote duniani uko
hapa hapa kwetu,"amesema Dkt. Magufuli.

 

No comments :

Post a Comment