Tuesday, October 6, 2020

NHIF YAGEUKIA MAKUNDI MAALUM


 Meneja wa mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Arusha Isaya Henry Shekifu akizungumza na wadau wa NHIF ambao hawapo pichani mkoani arusha katika mkutano wa Viongozi wa Vyama vya ushirika kuhusu utaratibu wa kujiunga na mfuko huo pamoja na huduma zao.

 Baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wakifuatilia kwa makini Mjadala wa namna mfuko wa bima unavyofanya shughuli zake,huduma zilizopo na namna ya kujiunga.

Na.Ashura Mohamed - Arusha

Mfuko wa Bima ya afya nchini (NHIF) umetoa elimu kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika wapatao 300 kutoka wilaya tatu za mkoa wa Arusha,pamoja na kugawa kadi za bima ya afya zipatazo 107 kwa madereva pikipiki.

Akizungumza na wadau wa NHIF Meneja wa mfuko huo mkoa wa Arusha Isaya Henry Shekifu,alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbali mbali yanayofanya kazi pamoja.

Bw.Shekifu alisema kuwa wilaya hizo ni Pamoja na wilaya ya Arusha mjini,Meru na Arusha Vijijini.

Aidha alisema kuwa kumekuwepo na dhana nyingi potofu kuhusu mfuko wa bima ya afya na utaratibu wa kujiunga kwa makundi hayo, ambayo sio rasmi hivyo wameona ni vyema kutoa elimu sahihi kwa watu sahihi ili waweze kutambua vifurushi vya huduma zilizopo.

“Leo tumekutana na Viongozi wetu hawa wa Vyama vya Ushirika kama AMCOS juu ya bidhaa yetu ya Ushrika Afya,ambayo kila mwanachama anatakiwa alipie shilingi 76,800 lakini pia makundi mbali mbali ya Madereva ambayo tumeyafungua kama Madereva Afya,tuna ndugu zetu hawa madareva wa Noah na Pikipiki ambao tumewapatia kadi leo”alisema bw.Shekifu.

Bw.Shekifu alisema kuwa mpango wa Ushirika Afya ni mpango mahsusi ulioanzishwa na Mfuko huo kwa wanachama wa vyama vya msingi vya Ushirika wa Mazao matano ya kimkati ambayo ni Chai,Pamba,Kahawa,Korosho na Tumbaku.

“Pia tumekutana na Viongozi wa wafanyabiashara wadogo ambao tunaita Wamachinga Afya pamoja na Umoja afya,kwahiyo haya makundi yote tumeona kupitia hawa viongozi tuhamasishane na tuzungumze kuhusu bima ya Afya ili waweze kujiunga na mfuko huu’’alisema Shekifu

Bw.Shekifu alisema kuwa Bima ya Afya kwa sasa wametanua wigo wa huduma na kuyafikia makundi yote,bila kuangalia anatokea kundi gani kwa kuwa hapo awali utaratibu wa kujiunga haukuwa rafiki tofauti na sasa.

Hata hivyo jumla ya vituo vya Afya vipatavyo 8500,nchini vinatoa huduma za afya ikiwa ni pamoja na matibabu yote ya msingi pamoja na huduma za dawa.

Nae bw.Gidioni Ndewario Palangyo kutoka Nkoaranga AMCOS,iliyopo wilayani Meru aliwataka wakulima kutumia fursa hiyo kujiunga na NHIF kwa kuwa ina manufaa makubwa kwao.

“Mimi kama mkulima wa kahawa pamoja na fedha zetu kuja awamu nimejikuta ninanufaika na huduma za afya pamoja na familia yangu,na hii inanipa uhakika kupata huduma za afya bila wasiwasi hata kama ikiwa ni gharama kubwa nina uhakika wa kutibiwa kwa kuwa ni mwanachama”alisema Bw.Ndewario

Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Arusha bw.Emmanuel Sanka aliwataka wakulima na makundi mengine kutokuangalia gharama za kujiunga kuwa ni kubwa bali wachangamkie fursa hiyo kwa kujiunga na kuwa wanachama kwa kuwa afya ni gharama.

 

No comments :

Post a Comment