Wednesday, October 7, 2020

Mke wa Rais wa Malawi afurahia maonesho ya Urithi wa asili na utamaduni Makumbusho ya Taifa Tanzania


Mhifadhi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Amandus Kweka akitoa maelezo kwa Wake wa Marais wa Jamhuri ya Malawi na Mama Monica Chakware Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Janeth Magufuli walipotemebelea chumba maalum cha kutunzia vitu vya thamani vya urithi wa asili na utamaduni wa Tanzania

Afisa Elimu Mwandamizi wa Makumbusho ya Taifa, Bibi Anamary Bagenyi akitoa maelezo kuhusu sanaa za sasa kwa wake wa Marais wa Jamhuri ya Malawi na Tanzania walipotembelea Makumbusho ya Taifa

Mke wa Rais wa Jamhuri ya Malawi mama Monica Chakwera na mwenyeji wake mke wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Pombe Magufuli wakifurahia jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga walipotembelea Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam

*************************************

Na Mwandishi Wetu

Mke wa Rais wa Malawi, Mama Monica Chakwera ametembelea Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam na kufurahishwa na uhifadhi wa urithi wa asili na wa utamaduni ikiwemo fuvu halisi la mwanadamu wa kale (Zinjanthropus).

Mama Monica Chakwera ambaye aliongozana na mwenyeji wake Mama Janeth Magufuli ametembelea onesho la Chimbuko la Mwanadamu eneo ambalo linaonesha masalia ya zamadamu wanaoitwa Zinjanthropus na homo habilis, masalia ya wanyama mbalimbali na zana za mawe za mwanzo zilizogundulika katika Bonde la Olduvai.

Vile vile aliweza kujionea fuvu halisi la mwanadamu wa kale lijulikanalo kama Zinjanthropus ambalo linatunzwa katika chumba maalum (strong room) katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni.

Mama Chakwera alijikuta akicheka baada ya mtoa maelezo, Dkt Agness Gidna kusema kuwa wanadamu wote duniani chimbuko lao ni Afrika kwa sababu ya ushahidi wa masalia ya mwanadamu ambayo yanaonesha binadamu aliishi zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita.

Mke wa Rais wa Malawi alitembelea pia ukumbi wa Sanaa za sasa na michoro ya kale ya miambani.

Wake wa Marais walipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dr Noel Lwoga, ambaye alithamini na kufurahia ujio wao makubmusho, na kusisitiza wananchi wa Tanzania na Wageni kutoka nchi mbalimbali kutembelea Makumbusho ya Taifa na Malikale zilizopo nchini ili kujiongezea maarifa, kuburudika, kufahamu historia na asili yao, na kujivunia utajiri wa rasilimali za asili na za kitamaduni za nchi yetu.

Mama Monica Ckakwera yupo kwenye ziara ya siku tatu nchini Tanzania akiongozana na mumewe, Mhe Lazarus Chakwerwa. Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Chakwarwa yuko nchini kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kuimarisha urishirikiano baina ya nchi hizi mbili.

No comments :

Post a Comment