Waendesha baiskeli wakianza mashindano kutoka Shinyanga Mjini kuelekea Isaka (KM 150)
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi
imeendesha Mashindano ya Mbio za Baiskeli ‘CRDB SHINYANGA CYCLING
RALLY’ na kuendesha zoezi la Uchangiaji Damu Salama ikiwa ni sehemu ya
Maadhimisho ya Kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Maadhimisho hayo yalitawaliwa na
mbio za Baiskeli yaliyoleta burudani ya aina yake kwa wakazi wa mkoa wa
Shinyanga na maeneo Jirani yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB
ikishirikiana na wadau mbalimbali yakiongoza na kauli mbiu ya ‘Shinyanga Yetu, Damu Yetu’
yamefanyika Jumatano Oktoba 14,2020 katika Uwanja wa CCM Kambarage na
barabara ya Shinyanga kwenda Kahama ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.
Waendesha baiskeli walionesha
umahiri wao wa kuendesha baiskeli kwa kasi na umakini mkubwa katika
mashindano ya wanaume masafa marefu kwa umbali wa Kilomita 150 kutoka
Shinyanga kwenda Isaka, huku kundi jingine likiendesha baiskeli kwa
umbali wa kilomita 80 kutoka Shinyanga Mjini kwenda Kituli huku Wazee
kundi la wanaume wakizunguka uwanja wa CCM Kambarage mara 30 na wanawake
wakizunguka uwanja huo mara 25 na baada ya mashindano washindi kuanzia
wa kwanza hadi wa 10 wamejinyakulia zawadi ya fedha taslimu na medali.
Mshindi wa Kwanza Mbio za
Baiskeli za Kilomita 150 (Shinyanga- Isaka) alikuwa Gelard Nkonda kutoka
Shinyanga aliyejinyakulia kitita cha shilingi milioni 1 na
medali,mshindi wa pili Rashid Hamis kutoka Arusha aliyeondoka na kitita
cha sh. 700,000/= na medali,mshindi wa tatu George Izengo kutoka
Shinyanga aliyepata zawadi ya Shilingi 500,000/= na medali huku washindi
kuanzia wan ne hadi 10 wakipata zawadi ya shilingi 200,000/- na medali
kila mmoja.
Kwa upande wa mbio za kilomita
80 (Shinyanga – Kituli) mshindi wa kwanza ni Mwigulu Mdogo aliyepata
zawadi ya shilingi 400,000/- na medali, wa pili Dotto Mahega (sh.
200,000/- na medali), mshindi wa tatu Mwendokasi Kalikali (Sh. 100,000/=
na medali) na washindi wa nne hadi namba 10 wakiondoka na kifuta jasho
cha shilingi 30,000/- na medali kila mmoja.
Aidha kwa upande wa mbio fupi za
wanawake (kuzunguka uwanja wa Kambarage mara 25) mshindi wa kwanza
alikuwa Futi mbili Richard aliyeondoka na kitita cha shilingi 200,000/=
na medali,mshindi wa pili Modester Kashinje (sh. 100,000/- na medali, wa
tatu Grace Nchambi (sh . 50,000/= na medali huku mbio za wazee wanaume
(kuzunguka uwanja wa Kambarage mara 30) mshindi wa kwanza akiwa ni Sambo
wa Sambo aliyepata zawadi ya sh. 200,000/= na medali,wa pili Kabaya
Clement (sh. 100,000/- na medali, mshindi wa tatu Dotto Clement (sh.
50,000/- na medali).
Wakati mbio za baiskeli
zikiendelea zoezi la uchangiaji wa damu salama lilikuwa linaendelea
uwanjani huku mechi kali kati ya Timu ya mpira wa miguu ya Benki ya CRDB
na Bwalo Gymnastic Centre ikichezwa uwanjani ambapo CRDB waliwababua
Bwalo Gymnastic Centre bao 4-1 ambapo washindi na walioshindwa walipata
zawadi ya mbuzi watatu ambao waliwachoma na kula nyama choma.
Katika maadhimisho hayo,pia
Benki ya CRDB kwa kushirikiana na wadau wake wakiwemo Sanlam General
Insurance, Kampuni ya Jambo Food Products, NIC wametoa msaada Viakisi
Mwanga ‘Reflectors’ zenye thamani ya shilingi milioni 3.9 kwa ajili ya
waendesha bodaboda mkoa wa Shinyanga waliopo kwenye vituo 35
vilivyosajiliwa kupitia ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani
mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa
Maadhimisho hayo, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack
ameipongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu mkubwa katika shughuli mbalimbali
lakini kwa ushirikiano inaotoa kwa serikali na wadau mbalimbali wa
maendeleo.
“Nawashukuru sana Benki ya
CRDB kwa kuifanya siku ya leo kuwa ya Furaha badala ya majonzi
tukimkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hatutakiwa kulia bali tunatakiwa kusherehekea mambo mazuri yaliyofanywa
na baba wa Taifa ambaye nae pia alipenda kuendesha baiskeli”,alisema Telack.
“Wananchi wa Shinyanga
mmewapa furaha wananchi,tangu asubuhi kila mahali walipopita waendesha
baiskeli kuanzia hapa uwanja wa CCM Kambarage hadi Isaka,wananchi
wamejitokeza kwa wingi kuangalia mbio za baiskeli. Hakika mbali na
kuleta furaha pia mmewajenga vijana walioshiriki mbio za baiskeli kuwa
na nguvu na wakakamavu. Hizi mbio za baiskeli siyo lelemama, Niwapongeze
sana washiriki wote wa mbio za baiskeli”,aliongeza Telack.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo
wa Mkoa, aliwapongeza wananchi wote waliojitokeza kuchangia damu salama
na kufanikisha kupatikana kwa uniti 140 za damu akibainisha kuwa
wameokoa maisha ya wananchi wenye uhitaji wa damu na kuwaomba wananchi
kuendelea kuchangia damu.
Kwa upande wake, Meneja wa Benki
ya CRDB Kanda ya Magharibi Said Pamui alisema lengo la kuandaa
mashindano hayo ya mbio za baiskeli na kuendesha zoezi la uchangiaji
damu salama kuwa ni kuadhimisha Kumbukumbu ya Hayati Baba wa
Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini pia kama sehemu ya
mwendelezo wa kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Pamui aliwashukuru wadau
walioungana na Benki ya CRDB katika maadhimisho hayo ambao ni Jambo Food
Products CO.LTD,East African Spirit (T) Ltd, Fresho Investment Co. Ltd ,
Jielong Holdings Co. Ltd, Doctors With Africa,Tanzania Red Cross,
Sanlam General Insurance, Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga Kitengo Cha
Damu Salama,Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga na Karena
Hotels Ltd.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack akizungumza wakati wa
Maadhimisho ya Miaka 21 tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius
Kambarage Nyerere leo katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga
maadhimisho ambayo yameenda sanjari Zoezi la Uchangiaji Damu na
Mashindano ya Mbio za Baiskeli yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Said Pamui
akielezea lengo la mashindano ya mbio za baiskeli na uchangiaji damu
salama.
Meneji wa Benki ya CRDB Kanda ya
Magharibi, Said Pamui akiteta Jambo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Zainab Telack na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko
(kulia).
Waendesha baisekeli wakianza kutimua vumbi mjini Shinyanga kuelekea Isaka (KM 150)
Mshindi wa Kwanza Mbio za Baiskeli za Kilomita 150 (Shinyanga- Isaka) Gelard Nkonda akirejea Shinyanga Mjini kutoka Isaka
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe.
Zainab Telack akijiandaa kumvalisha Medali na kumkabidhi kitita cha
shilingi Milioni moja Mshindi wa Kwanza Mbio za Baiskeli za Kilomita 150
(Shinyanga- Isaka) Gelard Nkonda kutoka Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe.
Zainab Telack akimkabidhi mshindi wa kwanza mbio fupi za wanawake
(kuzunguka uwanja wa Kambarage mara 25) Futi mbili Richard kitita cha
shilingi 200,000/= na medali.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Saidi Pamui akizungumza wakati wa zoezi la kugawa Viaksi Mwanga
Mwakilishi
wa Sanlam General Insurance , Tamari Mbise akizungumza wakati wa kukabidhi
Viaksi Mwanga kwa ajili ya waendesha bodaboda
wa Sanlam General Insurance , Tamari Mbise akizungumza wakati wa kukabidhi
Viaksi Mwanga kwa ajili ya waendesha bodaboda
Meneja
wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Said Pamui akikabidhi Viaksi Mwanga kwa
Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga Africanus Sulle kwa ajili ya waendesha bodaboda mkoa wa
Shinyanga
wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Said Pamui akikabidhi Viaksi Mwanga kwa
Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Shinyanga Africanus Sulle kwa ajili ya waendesha bodaboda mkoa wa
Shinyanga
Katibu
Tawala Msaidizi Mkoa wa Shinyanga Joachim Otaru na viongozi wa Benki ya
CRDB akipiga picha na kikosi cha timu ya Benki ya CRDB na Bwalo
Gymnastic Centre
Mchezo kati ya Timu ya Benki ya CRDB na Bwalo Gymnastic Centre ukiendelea ambapo CRDB waliibuka washindi
Wananchi wakiendelea kuchangia damu salama
Askofu wa kanisa la KKKT, Dk. Emmanuel Makala akiwa na mke wake wakati wakichangia damu salama
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe.
Zainab Telack akiongozana na viongozi mbalimbali kwenda kutembelea
mabanda ya wadau waliojitokeza na kushiriki katika maadhimisho ya
Nyerere Day
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
No comments :
Post a Comment