Saturday, October 10, 2020

BALOZI SEIF AIPONGEZA TASAF KWA UTENDAJI KAZI BORA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi  na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania
{Tasaf}  Ladislaus Mwamanga wakifungua na kuweka Jiwe
la Msingi la Ofisi ya Utawala  pamoja na Jengo la Madarasa matatu ya
Skuli ya Sekondari ya Mahonda.

Balozi Seif Ali Iddi akitoa maelezo kwa wasimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Utawala la Skuli ya Sekondari ya  Mahonda mara baada ya kuweke Jiwe la Msingi Jengo hilo pamoja na  madarasa matatu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizungumza naWananchi,Walimu na Wanafunzi wa Shehia za Mahonda na Mkataleni kwenye hafla ya Uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi wa Ujenzi wa Jengo la madarasa matatu na jengo  la Utawala la Skuli ya Sekondari ya Mahonda.
Sehemu ya wananchi wakifuatilia mkutano huo

 MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Mfukowa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} umeonesha muelekeo mzuri wa ufanisi mkubwa

unaopatikana katika Utekelezaji wa Miradi ya Jamii tangu ulipoanzishwa ndani ya Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema Viongozi wa Wilaya, Halmashauri, Majimbo, Wadi pamoja na
Shehia wana wajibu na jukumu la kuwasimamia vyema wananchi katika
kuona miradi wanayoiibua katika Maeneo yao inaendelea kupata ufanisi
kama inavyojidhihirisha hivi sasa katika mpango huo unaosaidia
kustawisha Jamii.

Balozi Seif ameyasema hayo, wakati akizungumza na wananchi
wa Shehia za Mkataleni na Mahonda, Walimu na Wanafunzi mara baada ya
kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Madarasa Matatu pamoja na
Jengo la Utawala la Skuli ya Sekondari ya Mahonda  Miradi
inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf}.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ililazimika kufanya
mabadiliko katika ngazi ya Utawala kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) kwa upande wa Zanzibar ili kuona Taasisi hiyo ya Kijamii
inatekeleza wajibu wake katika misingi iliyopangiwa ya kuunga mkono
jitihada za Jamii kwenye Miradi yao ya Maendeleo.

Balozi Seif amebainisha wazi kwamba wapo baadhi ya Watendaji wa TASAF
katika kipindi kilichopita walikuwa wakizorotesha kazi kwa kufikiria
zaidi maslahi yao binafsi bila ya kujali kwamba chombo hicho
kimeanzishwa kwa lengo la kuwakomboa Wananchi Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea faraja yake kutokana na
Uzalendo mkubwa wa Watendaji na Viongozi wa Mfuko huo  na kuwapongeza
jinsi walivyojizatiti katika kusimamia Utekelezaji wa Miradi
iliyobuniwa na Jamii inayokwenda kwa kasi katika maeneo mbali mbali
Nchini.

“ Nikiri kwa dhati Kwamba majengo haya niliyoyawekea jiwe la msingi
hivi punde  yanaendelea kujengwa katika ubora unaokubalika katika fani
ya ujenzi na uharaka wake uliyofikia huwezi kuamini kama ni ya Mwezi
Mmoja.” Amesema Balozi Seif.

Amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sera
yake ya Elimu imejizatiti katika kuona Wanafunzi wote wa Visiwa vya
Unguja na Pemba wanapata taaluma katika mazingira bora na kiwango
kinachokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Akigusia Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki chache zijazo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu
ya CCM Taifa amewatahadharisha wana CCM na Wananchi wote nchini
kujiepusha kuingia katika mtego wa kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura.

Wakitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Tasaf Mkurugenzi mkuu wa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania  Ladislaus Mwamanga na
Mkurugenzi Uratibu wa Shughuli za Serikali Zanzibar anayesimamia TASAF
Zanzibar Khalid Bakari Amran wamesema Zanzibar  itapatiwa
Shilingi Bilioni 112 katika Kipindi cha Miaka minne ijayo.

Mradi wa ujenzi wa Jengo la madarasa matatu ya Skuli ya Sekondari
Mahonda utagharimu zaidi ya Shilingi Milioni sabini ya saba
wakati la Jengo la Utawala likitegemewa kugharimu jumla ya
Shilingi Milioni 78 Nukta Nane.

 

No comments :

Post a Comment