Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu ameiteua Benki ya CRDB kuwa balozi
wa mazingira wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Pendezesha Tanzania
iliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya Goba, iliyopo Dar
es salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira).
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo iliyohudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar
Kunenge, Waziri Zungu aliipongeza Benki ya CRDB kwa utekelezaji wa
mikakati ya kusaidia jitihada
za Serikali katika kutunza na kuboresha mazingira kupitia kampeni hiyo
yaPendezesha Tanzania ambayo inahamasisha umuhimu wa upandaji miti
katika kutunza mazingira.
Waziri Zungu amesema kampeni ya Pendezesha Tanzania imekuja wakati
muafaka kwani inaenda sambamba na mkakati wa serikali wa kupanda miti
Milioni Moja na Laki Tano kwa kila Halmashauri kwa mwaka ili kutekeleza
Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame.
“Niipongeze Benki ya CRDB kwa ubunifu huu mliokuja nao wa kuwahamasisha
watanzania kutunza mazingira yao yaliyowazunguuka. Niwaahidi Serikali
itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tufikie lengo la
kuboresha na kuyatunza
mazingira yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Waziri
Zungu huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano Benki ya CRDB katika
kuweka kipaumbele suala la utunzaji wa mazingira.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge aliishukuru Benki
ya CRDB kwa kuzindua kampeni ya Pendezesha Tanzania katika mkoa wa Dar
es Salaam.
Kunenge aliwataka wananchi wa mkoa huo kupanda mti mmoja kila mtukatika makazi yao kama sehemu ya kutekeleza kampeni hiyo.
“Asanteni sana Benki ya CRDB kwa kutupa heshima wakazi wa Dar es Salaam
ya kutupendezeshea jiji letu. Niwaahidi kuwa tutashiriki kikamilifu
kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema
Kunenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela
alisema kampeni hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa sera ya benki hiyo
kusaidia shughuli za maendeleo katika jamii ambayo inaelekeza asilimia 1
ya faida kila
mwaka kusaidia nyanja za elimu, afya na utunzaji wa mazingira.
“Lengo la kuzindua kampeni hii ni kuendelea kuihamasisha jamii kuona
jukumu la kupanda miti ni la jamii nzima. Tumeanza kwa kupanda miti 2000
katika shule zote za msingi na za sekondari zilizo katika Kata ya Goba
kwa lengo la kuzifanya shule
hizi kuwa na mazingira bora na rafiki kwa watoto kusoma,” alisema Nsekela
Kampeni ya Pendezesha Tanzania inatarajiwa kufanyika nchi nzima ili
kusaidia kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupanda na kutunza miti
katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumeanza Dar es Salaam katika shule hizi zilizopo
katika kata ya Goba, lakini lengo letu ni kufika katika wilaya na vijiji vyote Tanzania,” aliongezea Nsekela.
Sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Pendezesha Tanzania, Benki ya CRDB
pia imetoa msaada wa pampu za maji kwa shule za Sekondari za Fahari,
Goba na Kinzudi ili kusaidia kuboresha upatikanaji wa maji katika shule
hizo.
Akizungumza juu mikakati ya biashara inayozingatia mazingira, Nsekela
alisema Benki ya CRDB imejiwekea mfumo wa biashara ambao unazingatia
utunzaji wa mazingira ikiwamo kuweka sera inayoelekeza utoaji wa mikopo
kwa miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira, kuanzisha huduma na
bidhaa za kidijitali, pamoja na kuwekeza katika mifumo ya ufanyaji kazi
inayopunguza matumizi ya karatasi.
Afisa elimu kata ya Goba, Edward Shilamba aliishukuru Benki ya CRDB kwa
kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti katika shule za Sekondari na
Msingi kata ya Goba. Afisa elimu huyo alimhakikishia Waziri wa Mazingira
kuwa wataweka
mikakati madhubuti ya kuhakikisha miti hiyo inastawi kama inavyotarajiwa.
Kutokana na jitihada za kusaidia utunzaji mazingira mpaka, mwaka 2019
Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki
na Kati kuweza kutambuliwa na kupata usahili katika Mfuko wa Umoja wa
Mataifa unaoshugulikia
masuala ya Tabia Nchi “United Nations Green Climate Fund (GCF)”.
Kupitia usahili huu, Benki ya CRDB sasa inaweza kushiriki katika
kuwezesha miradi mikubwa ambayo ni rafiki wa mazingira, kwa kutoa mikopo
ya hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge akizungumza wakati wa
uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha watanzania
kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania" inayoendeshwa na
Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya
Shule ya Sekondari Goba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza
wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira kwa kuhamasisha
watanzania kupanda miti ijulikanayo kama “Pendezesha Tanzania"
inayoendeshwa na Benki ya CRDB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana
kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Goba.
No comments :
Post a Comment