Waziri Hasunga amesema pamoja na Serikali kuweka juhudi kubwa katika kuboresha sekta ya kilimo nchini, ni dhahiri kuwa bado wapo wakulima, hususan wakulima wadogo, ambao wamekuwa wakifanya kilimo duni kutokana na wengi wao kutomudu gharama za uendeshaji wa kilimo cha kisasa. Jambo ambalo linahitaji ushiriki wa taasisi za fedha na wadau wengine wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo kimtaji wakulima hao na kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo.
“Nikiwa
Waziri mwenye dhamana ya kilimo nimefurahishwa sana na ushirikiano huu
wa utoaji wa huduma za uwezeshaji wakulima baina ya Benki ya CRDB na
Kampuni za ETC Agro, LoanAgro na Agricom ambao unauzinduliwa rasmi leo
hii. Uhusiano ambao unakwenda kuleta manufaa kwa wakulima kwa
kuwawezesha kupata mikopo nafuu ya vifaa vya kilimo ikiwamo matrekta,
power tiller, mashine za kuvunia na nyinginezo” alisema Waziri Hasunga.
Pamoja
na matumizi ya zana za kilimo, Waziri Hasunga amewaomba wakulima
kujikita katika kilimo cha kisasa kwa kuhakikisha wanaanza na utafiti wa
masoko kabla ya kulima ili kujihakikisha uhakika wa kuuza mazao yao
baada ya mavuno badala ya kuanza kulima bila kufahamu mahitaji ya soko
na hivyo kuishia kutegemea serikali katika kutafuta masoko. Sambamba na
hilo amewaomba makampuni na wanunuzi kuweza kuwekeza katika kilimo cha
mkataba ili kuwahakikishia soko wakulima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameshauri Watanzania kujikita zaidi kwenye kilimo cha kisasa ili kuongeza tija na hivo kukuza kipato chao na taifa kwa kwa ujumla huku akisema Benki ya CRDB imejipanga kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa zana za kilimo kwa kushirikiana na kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom.
“Kama
unavyofahamu Mheshimiwa kuna taasisi za fedha zaidi ya 58 nchini na kwa
ujumla wao wanatoa asilimia 60 ya mikopo yote ya sekta ya kilimo wakati
Benki ya CRDB pekee inatoa asilimia 40. Hii inadhihirisha adhma ya
Benki ya CRDB ya kuunga juhudi za serikali za kuwaletea Watanzania
maendeleo kwa vitendo kwa kuzingatia kuwa sekta ya kilimo inatoa ajira
kwa takribani asilimia 75 ya Watanzania huku ikichangia asilimia 28
kwenye pato la Taifa” Alisema Nsekela.
Nsekela
alisema Benki ya CRDB inataka kuona mkulima ananufaika na juhudi zake
na ndio maana Benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni za ETC Agro, Loan
Agro na Agricom zimeungana kutoa mikopo hiyo ya zana za kilimo ambayo
imezingatia mahitaji na uhalisia wa mazingira ya mkulima wa Kitanzania.
“Tumepunguza
riba ya mkopo kutoka asilimia 20 iliyokuwa ikitozwa hapo awali hadi
kufikia asilimia 18, Tumepunguza kiwango cha gharama ya awali ya
manunuzi kutoka asilimia 35 iliyokuwa ikilipwa na mteja hadi kufikia
asilimia 25, ambapo hivi sasa asilimia 75 iliyobaki italipwa na Benki
kama mkopo,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa sasa hivi mteja hata
hitajika kuleta dhamana yoyote kwa ajili ya mkopo ambapo zana hizo
zitatumika kama dhamana.
Mbali
na matrekta mikopo hiyo ya zana za kilimo inajumuisha power tiller kwa
ajili ya kulimia, combine harvester kuvunia, na zana nyinginezo,
ambapo mteja anaweza kuchukua mkopo hadi wa shilingi bilioni 3 kwa
kipindi cha miezi 36 hadi miezi 60.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Agricom, Bi. Angelina Ngalula ambao ni mmoja katika washirika wa Benki ya CRDB katika mikopo hiyo amesema wanaona ndoto yao ya kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini inakwenda kutimia kwa kupitia ushirikiano huo na Benki ya CRDB.
Bi.
Ngalula amesema kuwa kampuni yao imeanza kufanya uzalishaji wa zana za
kilimo nchini kupitia vijana wa Kitanzania ili kuchangia katika
upatikanaji wa ajira. Kampuni hiyo inatarajia katika kipindi cha mwaka
mmoja kuuza power tiller 500 ambazo zinahitaji trela 500 na trela zote
hizo zitazalishwa nchini na kuchangia kutoa ajira kwa vijana wa
Kitanzania.
Hadi sasa Benki ya CRDB imeshatoa mikopo ya zaidi ya
shilingi trilioni 1.6 kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani katika
kilimo, mikopo hii imeelekezwa katika maeneo kama vile; pembejeo na
uendeshaji, zana za kilimo, ujenzi wa maghala, uunganishwaji na masoko
na uwekezaji kwenye viwanda.
No comments :
Post a Comment