Meneja wa SIDO mkoa wa Singida, Agnes Yesaya akitoa maelezo mafupi juu ya Mafunzo hayo
Mkufunzi wa somo la ukarabati na uimarishaji wa vyerehani, Dickson
Shenkalwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida, Eng Paskasi
Muragili juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili mafundi vyerehani
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Eng Paskasi Muragili akikabidhi Cheti cha
kuhitimu Mafunzo ya Ujasiriamali kwa mmoja ya washiriki, Zainabu Saidi
ambaye ni mlemavu wa viungo kwenye hafla ya ufungaji Mafunzo hayo.
Na Abby Nkungu, Singida
WAJASIRIAMALI wadogo mkoani Singida wametakiwa kuwa na nidhamu ya
matumizi ya fedha wanazopata ili kuweza kukuza mitaji yao na
kujiimarisha zaidi kiuchumi.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskasi Muragili
wakati wa hafla fupi ya kufunga Mafunzo ya Wajasiriamali 68 kutoka
maeneo mbalimbali ya mkoa huo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Shirika la
kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mjini Singida.
Alisema wajasiriamali wengi hupata vipato vya kutosha kupitia shughuli
zao mbalimbali za kila siku lakini kutokana na kutokuwa na nidhamu ya
matumizi ya fedha hizo na kutojiwekea malengo, mara nyingi hujikuta
hawana fedha kila wanapohitaji kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
"Huenda kinachochangia zaidi ni ukosefu wa elimu ya biashara kwa
wajasiriamali hao hali inayosababisha washindwe kuweka kumbukumbu za
mapato na matumizi ya fedha zao" alisema na kuongeza;
Mali bila daftari, hupotea bila habari. Huo ndio ukweli usiofichika.
Ninyi mmepata bahati ya kufundishwa somo la Usimamizi wa biashara wakati
wa mafunzo yenu hapa SIDO. Tumieni vyema ujuzi huo kwa kutunza
kikamilifu mahesabu yenu ya kila siku ili kujitofautisha na wale ambao
hawajapata elimu hiyo".
Awali, Meneja wa SIDO mkoa wa Singida Agnes Yesaya alieleza kuwa
wahitimu hao walipata fursa ya kujifunza namna ya kukarabati vyerehani
vyao na elimu ya awali ya biashara; hivyo akawataka waende kuwa chachu
ya maendeleo kwenye maeneo yao ya kazi na kueneza habari njema za SIDO.
Naye mkufunzi wa somo la ukarabati na uimarishaji wa vyerehani, Dickson
Shenkalwa alisema kuwa wengi wa washiriki wa mafunzo hayo hawakuwa na
ujuzi wa kutosha juu ya zana wanazotumia.
"Wamekuwa wakiwaita mafundi ili kuwarekebishia hitilafu zinazojitokeza
lakini kutokana na mafundi hao kutokuwa na ujuzi wa kutosha au kutaka
kujipatia vipato vya kinyemela, matengenezo yanayofanyika huwa
hayadumu.
Wenye vyerehani huendelea kugharamia siku hadi siku huku wakichelewa
kumaliza kazi za wateja wao.... Sasa, hawatakumbana na changamoto hizo
tena", alisema.
No comments :
Post a Comment