Tuesday, September 1, 2020

UTSS kufadhili wanafunzi 18 wenye ualbino

Meneja kitengo cha elimu wa Shirika la Under The Same Sun, (UTSS) Grace Wabanhu katikati akiwa katika picha na Marko Sein kushoto na Amina Selemani, wakionyesha laptop walizopatiwa na Shirika hilo kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo kabla ya kwenda Chuoni.
Meneja kitengo cha elimu wa Shirika la Under The Same Sun, (UTSS) Grace Wabanhu kushoto, akimkabidhi laptop mmoja wa wanafunzi  Amina Selemani, walizopatiwa na Shirika hilo kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo kabla ya kwenda Chuoni.
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

Shirika la Under The Same Sun (UTSS) limejipanga kugharamia mafunzo ya kujiandaa na elimu ya juu kwa wanafunzi 18 wenye ualbino walio katika programu ya ufadhili wa elimu ili kuwajengea uwezo wa kutambua wajibu wao wawapo vyuoni.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za UTSS , kwa niaba ya Mkurugenzi,  Meneja wa kitengo cha Elimu cha Shirika hilo, Grace Wabanhu amesema, mbali na mafunzo pia wanafunzi hao kila mmoja atapatiwa kompyuta mpakato (Laptop) ili kuwawezesha kujisomea kwa karibu  hasa kwa wao ambao wamekuwa na uono hafifu.

Wabanhu amesema, lengo kubwa la mafunzo hayo ambayo yanafadhiliwa na Vivuan Grace Ash na Open Chapel Society za nchini Canada ni kuwapa fursa wanafunzi hao kutambua mfumo wa elimu ya vyuo vikuu wanayokwenda kukutana nayo ambao unataka mwanafunzi kujua jinsi ya kujitegemea na kufanya maamuzi sahihi wakati wote ili kila mmoja aweze kutimiza malengo yake.

 "Mafunzo haya  yatawahamasisha na kuwakumbusha vijana hawa juu ya wajibu uliombele yao wa kuendelea kuwa waadilifu, wenye kujituma, na kuweza kutimiza malengo yao na ndoto zao ili kuithibitishia jamii kwamba watu wenye ualbino na ulemavu wanaweza kurudisha thamani na fadhila katika jamii", amesema Wabanhu.

 Aidha, shirika hilo limewapongeza wahitimu wote wenye ulemavu waliweza kufanya vema kwenye mitihani yao ya kitaifa hasa katika kidato cha nne na cha sita kwani ufaulu kwao ni chache na hamasa kwa wenzao wenye ulemavu, familia, ndugu jamaa, marafiki n nchi nzima kwa ujumla.

"Hii ni awamu ya tano kwa mafunzo haya kufanyika tangu yalipoanzishwa mwaka 2018  ambapo mpaka sasa vijana 91 kutoka ngazi na mikoa mbali mbali wamefikiwa na mpango huu ambapo kwa kipindi cha miaka 12 UTSS imeshatoa na kufadhili masomo kwa wanafunzi wenye ualbino 429 waliopata udahili kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu".

Pia Wabanhu ameto wito kwa wadau mbali mbali wa masuala ya elimu na ulemavu kuendelea kuipa kipaumbele na kuipambania Agenda ya ujumuishi katika kila ngazi ya jamii kuanzia ile ya familia.

No comments :

Post a Comment