Afisa
wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Hamisi Duma akiwaeleza wadau
watarajiwa kuhusu jinsi wakulima wanavyoweza kujiunga uanachama, walipotembelea
banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Nanenane Mkoani Simiyu. (Na Mpigapicha
Wetu)
Na Christian Gaya Majira Ijumaa 28 Agosti 2020
Idadi
kubwa ya Watanzania mpaka sasa bado wanaamini ya kuwa, hifadhi ya jamii ni
stahili ya wafanyakazi walioajiriwa pekee, tena...
wale wenye vipato vidogo.
Kabla
ya kuwa na sera ya hifadhi ya jamii na kabla ya mabadiliko ya sheria za hifadhi
ya jamii kuwa mifuko kamili ya hifadhi ya jamii, sheria nyingi zilikuwa
haziwajumuishi wafanyakazi kutoka katika sekta isiyo rasmi sheria hizo
zilizokuwa zimepitwa na wakati zilishughulika na wafanyakazi walioajiriwa na
kupata mshahara kwa mwezi tu.
Na kwa ajili ya kupanua wigo zaidi wa hifadhi
ya jamii na kwa kisheria ya kuwa hifadhi ya jamii ni haki ya kila mtu hivyo
basi mtu yeyote aliyejiajiri, mkulima, mchimbaji madini mdogo, mfanyakazi wa
ndani, pamoja na wafanya biashara wadogo wanatakiwa kujiandikisha kwa lazima au
kwa hiari na kulipa kadri ya uwezo wao ili kupata mafao yote yatolewayo na mIfuko
ya hifadhi ya jamii.
Baada ya mabadiliko ya sheria
ya mwaka 2018 ya mifuko ya hifadhi ya jamii, NSSF hivi sasa inahusika na sekta
binafsi na sekta isiyo rasmi inayojumuisha wakulima, wavuvi, wafugaji na
wajasiriamali ambao wote wanatakiwa kujiunga na shirika hilo na kuchangia kila
mwezi.
Hivyo kisheria mfuko wa NSSF ndiyo mpango wa
taifa wa hifadhi ya jamii kwa Tanzania Bara, unaotegemewa kushughulika na
wafanyakazi wote walio katika sekta binafsi walioajiriwa na makampuni au
taasisi za kitaifa na za kimataifa zisizo za kiserikali na ofisi zote za balozi
zinazoajiri.
Pamoja na ZVSSS
kwa upande wa Zanzibar ambao umeanzishwa na mfuko wa hifadhi ya jamii wa ZSSF
kwa ajili ya kupanua wigo wa uwanachama kwa kuandikisha wananchi
waliojiajiri kwenye sekta isiyo rasmi
kwa upande wa Tanzania Visiwani.
Jukumu
kubwa la mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni kuhakikisha ya kuwa inakuwa na
mikakati mahususi ya kuondoa fikra ndani ya vichwa vya idadi kubwa ya
watanzania kwa kuwaeleza ya kuwa hivi sasa hifadhi ya jamii haina ubaguzi wa
aina yeyote, kwa sasa hifadhi ya jamii ni fursa huru kwa wote, kwa walioajiriwa
na kwa wale waliojiajiri.
NSSF inatakiwa
kujipanga kwa makusudi ya kuhakikisha ya inawaelemisha wananchi wote walio
kwenye sekta isiyo rasmi na hata watu binafsi kuwawekea utaratibu wa wao
kujiunga, kuchangia na kunufaika.
Mfuko
wa NSSF unatakiwa kuonesha kwa vitendo na kwa mifano hai kutoka kwa wakulima,
wanafunzi, wavuvi na wajasiriamali namna wanavyochangia na wanavyofaidika huko
mijini na vijijini bila ubaguzi.
Inajulikana
wazi ya kuwa watanzania wanatambua ya kuwa wengi wao wapo katika sekta ya
kilimo na sekta isiyo rasmi ambao kwa vipato vyao wanavyopata wangeweza
kujiunga na mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii nchini.
Uzoefu
huu unashawishi ya kuwa mfuko wa NSSF sasa utazame katika sekta ya kilimo na
wachimbaji wa madini nchini.
Kilimo
ndio sekta mama ya uchumi wetu na mpaka sasa inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wetu, lakini
ukuaji wake ni asilimia 4.4
ambayo ni chini ya kiwango kinachotakiwa cha asilimia 6 kwa mwaka kutokana na kukosa uwekezaji wa kutosha.
Utafiti
wa hivi karibuni unaonesha ya kuwa mifuko hii kwa mipango yao mbalimbali ya
hifadhi ya jamii iliweza kuwafikia wakulima wapatao 29,000 na wachimbaji madini 7,000 na waliweza kujiunga na baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii
nchini kwa wakati huo.
Na baadhi
yao mpaka sasa wanaendelea kunufaika na mafao yanayotolewa yakiwemo ya muda
mrefu na ya muda mfupi ikiwemo na mikopo ya gharama nafuu kwa kupitia Benki ya
Azania.
Kwa
takwimu hizi za utafiti zinaonesha ya kwamba wananchi wengi wamekosa elimu ya
hifadhi ya jamii na taarifa sahihi juu ya utendaji wa mifuko hii ya hifadhi ya
jamii.
Ikumbukwe
ya kuwa hifadhi ya jamii katika nchi hii si jambo jipya au la kigeni, hata
katika jamii zetu kabla ya kuja kwa mifumo hii rasmi ya hifadhi ya jamii,
kulikuwepo na utaratibu wa jamii kujiwekea mifumo ya hifadhi ya jamii isiyo
rasmi na mpaka sasa inafanya kazi vizuri na kutoa huduma nzuri ya kinga ya
hifadhi ya jamii.
Katika
jamii zetu kulikuwepo na utaratibu wa kuwahudumia wazee, wasiojiweza na watoto
mpaka leo ndani ya makabila na familia zetu za kitanzania bado zinaendelea
kutoa huduma hizi za hifadhi ya jamii ingawa kwa kiasi fulani zimeathiriwa na
ujio wageni na nguvukazi kubwa kuhamia mijini kutafuta kazi za kuajiriwa.
Mtu
hakupoteza heshima na thamani yake katika jamii kwa kuwa amepoteza uwezo wake
wa kuchangia katika jamii, ama kwa kustaafu, kwa ajali au kwa kutojaaliwa uwezo
wa kuchangia.
Mabadiliko
ya kidunia yameifanya mifumo hii ya hifadhi ya jamii isiyo rasmi sasa isiweze
kuhimili jukumu hilo la kutoa kinga ya hifadhi ya jamii kwa wale wazee, akina
mama wajawazito, walemavu, wajane, wagane, watoto yatima, na wengineo.
Hivyo,
mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii ndio mbadala na salama ya ustawi wa
jamii au mtu katika dunia ya leo kuanzia tumboni mwa mama yake, utotoni, ujana,
mpaka utu uzima. Utafiti unaonesha pia ya kuwa mara nyingi shida na majanga huwafika
watu wakati ambao hawajajiandaa vema.
Na
ikumbukwe wazi ya kuwa maandalizi ya kustaafu huaanzia pale unapoanza kufanya
kazi uwe umeajiriwa au umejiajiri kwenye sekta iliyo rasmi au isiyo rasmi.
Moja
kati ya changamoto kubwa iliyo mbele watu wote ni jinsi ya upatikanaji na
uendelevu wa kipato cha kukidhi mahitaji ya maisha baada ya kustaafu.
Na
hapa haijarishe wewe ni mtumishi wa umma, mfanyakazi uliyeajiriwa kwenye sekta
rasmi au uliyejiajiri mwenyewe kwenye sekta isiyorasmi
Kustaafu
kunaweza kumaanisha kuondoka katika ajira rasmi yaani kufikia tamati ya ajira yako au kufikia
umri wa kustaafu kwa hiyari au kwa lazima.
Na kwa upande mwingine kustaafu ni kuondoka au
kuondoshwa katika ajira hususan kwa sababu ya umri kisheria au kufikisha tamati
ya mkataba wako.
Kuanza
kufikiria kustaafu ni jambo la lazima kwa kila mfanyakazi uwe umejiajiri au
umeajiriwa hivyo ni jambo ambalo huwezi kuliepuka hata kidogo katika maisha ya
hapa duniani.
Mwandishi
wa Makala hii ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa
masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea hakipensheni
website, Simu +255 655 13 13 41,
info@hakipensheni.co.tz
No comments :
Post a Comment