Mkurugenzi wa Leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania
(TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka akizungumza kwenye Mkutano wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni ‘Online
Content Service Providers’ uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya
mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2020 leo Jumanne Septemba 15,2020
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watoa huduma ya habari
mtandaoni kuhakikisha waandika habari sahihi na bila kuegemea upande
wowote hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa
Tanzania mwaka 2020.
Mhandisi Kisaka ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 15,2020 wakati
akitoa mada kuhusu Kanuni za Utangazaji wakati wa uchaguzi za mwaka 2015
kwenye Mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Watoa Huduma ya
Habari Mitandaoni ‘Online Content Service Providers’ uliofanyika katika kituo cha mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
"Muwe makini mnapoandika habari, usiegemee upande mmoja.
Unaporipoti hakikisha hujaongeza mtazamo wako,usiongeze ongeze maneno
yako. Hakikisha unawapa nafasi sawa wagombea wote wa vyama vya siasa",alisema Mhandisi Kisaka.
"Usitoe nafasi kwa mgombea anayetumia lugha kali na chafu inayoweza
kuhatarisha amani ya nchi. Kamwe chombo chako cha habari kisitumike
kuhamasisha au kuonesha kitu cha hovyo. Ukiona kitu cha hovyo unaweza
kukatisha matangazo",aliongeza Mhandisi Kisaka.
Akifungua Mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi Dkt. Wilson Charles amewataka Watoa Huduma ya Habari Mitandaoni
kuvipa nafasi sawa vyama vyote vya siasa na kuepuka kuandika habari
zenye kuhamasisha vurugu na kusababisha uvunjivu wa amani.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi tunavipongeza vyombo vya habari mtandaoni
kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkitupatia. Tumewaita ili kuwajengea
uelewa kuhusu mkachato wa uchaguzi,tunaamini kuwa mna nafasi kubwa ya
kuelimisha jamii kuhusu taratibu mbalimbali za uchaguzi ikiwa ni pamoja
na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenda kupiga kura Oktoba 28,2020”,amesema Dkt. Charles.
Mkutano huo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Watoa huduma ya habari
Mtandaoni wanaoendesha Blogu na Runinga za mtandaoni uliolenga kujadili
masuala mbalimbali ya mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2020 ili
kuwajengea uwezo watoa huduma ya habari mtandaoni kuhusu masuala ya
uchaguzi ili waweze kuandika habari kwa usahihi na kulinda amani ya
nchi.
No comments :
Post a Comment