Friday, September 4, 2020

TANZANIA YAIHAKIKISHIA UINGEREZA NA JUMUIYA YA KIMATAIFA UCHAGUZI HURU, HAKI


Balozi mteule wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam
Balozi mteule wa Uingereza nchini Mhe. David Concar akimkabidhi nakala ya hati za utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi
Balozi mteule wa Pakistan nchini, Mhe. Mohhamed Salim akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi  
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Pakistan nchini, Mhe. Mohhamed Salim Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge (kulia) akifuatilia maongeza mara baada ya Mabalozi wateue kuwasilisha hati za utambulisho kwa Waziri Prof. Kabudi.
************************************
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeihakikishia Uingereza pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa uchaguzi
mkuu unaotegemewa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2020 utafanyika kwa amani,uhuru na haki.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi mteule wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar  
Prof Kabudi amesema kuwa paamoja na mambo mengine, amemhakikishia balozi wa Uingereza nchini Mhe. Concar kuwa mchakato wa uchaguzi nchini unaendelea vizuri sana ambapo mikutano ya kampeni imeanza kwa ngazi zote (ngazi ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani) na mpaka sasa kampeni zinaendea vizuri.
“kama ilivyoada ya watanzania nimemhakikishia kuwa uchaguzi huu utafanyika kwa amani na utulivu na mwisho wa siku maamuzi yatakayotolewa na watanzania ya kuamua nani awe diwani, nani awe mbunge na nani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yataheshimiwa na watanzania wote,” Amesema Prof. Kabudi.
Kwa upande wake Balozi mteule Mhe.David Concar amesema kuwa katika maongezi yao mbali na kugusia suala la uchaguzi pia wameongelea namna ya kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Uingereza na mazingira bora ya kuvutia zaidi wawekezaji kuja nchini,kukuza biashara hususani baada ya Uingereza kujitoa katika jumuiya ya Umoja wa Ulaya na pia kusaidia maendeleo katika maeneo ya afya,maji pamoja na elimu.
Katika hatua nyingine Prof. Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Pakistan hapa Nchini Mhe. Mohamed Saleem.
Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi amesema kutokana na Pakistan kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika viwanda vya mbolea wamekubaliana kuangalia namna ya kushirikiana ili kujenga viwanda vingi vya mbolea hapa nchini pamoja na kufanya biashara ya moja kwa moja ya zao la chai badala ya kupitia katika masoko ya minada ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Balozi wa Pakistan nchini, Mhe. Mohhamed Salim amesema atahakikisha kuwa Tanzania na Pakistan zinaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi zote mbili ili kuweza kunufaika na furza za kukuza uchumi.
Hafla ya mabalozi wateule kukabidhi hati za utambulisho pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge.  

No comments :

Post a Comment