Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati) akipokea
Hundi ya Mfano ya shilingi bilioni 18.99, kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi wa Airtel-Tanzania, Bw. Gabriel Malata, ambayo ni sehemu
ya shilingi bilioni 32.9 ambazo Airtel imeilipa Serikali ikiwa ni gawio
na michango ya maendeleo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020. Wanaoshuhudia
kuanzia kulia ni Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbutuka, Katibu Mkuu
Wizara ya Mawasiliano, Dkt. Zainabu Chaula na Mkurugenzi Mtendaji Airtel
Tanzania, Bw. George Mathen (kushoto)
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akizungumza wakati
wa halfa ya kupokea gawio na michango kutoka Kampuni ya Airtel
Tanzania, ambapo Serikali imepokea kiasi cha Sh. Bilioni 32.99 jijini
Dodoma, zikiwemo shilingi bilioni 18.99 za gawio na shilingi bilioni 14
za michango ya maendeleo, Hafla ya makabidhiano imefanyika Jijini
Dodoma.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata,
akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gawio na michango ya maendeleo
kwa Serikali, Jijini Dodoma. Serikali inamiliki asilimia 49 ya hisa
katika Kampuni hiyo na Kampuni ya Bharti Airtel inamiliki asilimia 51.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (wa kwanza kushoto)
akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Kampuni ya
Airtel Tanzania Bi. Beatrice Singano akifafanua jambo baada ya Kampuni
hiyo kutoa gawio na michango ya maendeleo kwa Serikali yenye thamani ya
shilingi bilioni 32.99. Kuanzia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel
Tanzania Bw. George Mathen, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Airtel Bw.
Gabriel Malata na wa tatu kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Benny Mwaipaja, katika hafla
iliyofanyika jijini Dodoma.
Meza
Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James
(katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara hiyo
baada ya Serikali kupokea gawio na michango ya maendeleo yenye thamani
ya Sh. bilioni 32.99 kutoka Kampuni ya Airtel Tanzania jijini Dodoma.
*****************************************
Na. Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Kampuni ya Simu
za Mkononi ya Airtel Tanzania Plc, imeilipa Serikali ya Tanzania,
shilingi 32.9 bilion kama gawio na mchango maalum wa maendeleo baada ya
kupata faida katika
Mwaka wa Fedha 2019/20.
Mfano wa Hundi
mbili za fedha hizo Fedha hizo ziliwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Airtel Tanzania Plc, Bw. Gabriel Malata na kupokelewa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ndiye mlipaji Mkuu
wa Serikali, Bw. Doto James, Jijini Dodoma.
Akikadidhi hundi
hiyo, Bw. Malata alisema katika kiwango hicho cha shilingi bilioni
32.99, shilingi bilioni 18.99 ni gawio na shilingi bilioni 14 ni mchango
maalum wa maendeleo kwa Serikali baada ya Kampuni hiyo kupata faida ya
bilioni 38.5 kwa mwaka unaoishia Disemba 2019/2020.
Akielezea
mafanikio yaliyosababisha Kampuni yake kutoa gawio nono na michango ya
maendeleo ya shilingi bilioni 1 kila mwezi, Bw. Gabriel Malata alisema
licha ya uwekezaji mzuri katika upanuzi wa mtandao, idadi ya wateja
imeongezeka kutoka milioni 11.4 Machi 2019 mpaka 13.3 milioni Machi 2020
na kwa sasa umiliki wa soko ni asilimia 27 kwa taarifa ya Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Aliongeza kuwa
Airtel Tanzania Plc imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 500 huku
wanafanyakazi wa kigeni wakiwa saba tu na kupitia kampuni hiyo,
Watanzania 350,000 wamejiajiri kwa kuuza huduma za kampuni ya Airtel
Tanzania Plc kama vile kuuza vocha, mawakala wa Airtel Money hivyo
kuchangia maendeleo ya uchumi kwa kulipa ushuru kwa Serikali
Na kwa kuunga
mkono maendeleo ya serikali kama elimu na afya, Airtel pia imetoa 2.3
bilioni kwenye ujenzi wa Hosptili mkoani Dodoma na kwa kushirikiana na
Mamlaka ya Elimu Tanzania (VETA) kuzindua elimu kwa mtandao kupitia
applikesheni ya VSOMO ambapo wanafunzi zaidi ya 500 wamehitimu.
Akizungumza
katika hafla hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James
alisema tukio hilo la Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel kutoa gawio
na mchango wa maendeleo wa shilingi bilioni 32.99 ni la kihistoria baada
ya Serikali na Kampuni hiyo kuingia makubaliano maalumu ya kiutendaji
na kiumiliki yaliyofanyika mwaka 2019.
“Baada ya
majadiliano makali nay a muda mrefu, hatimaye Kampuni ya Bharti Airtel
ilikubali kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49
na Bartel imebakiwa na asilimia 51” alifafanua Bw. James.
Aliipongeza
Kampuni ya Airetl Tanzania kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha gawio cha
cha shilingi bilioni 18.99 na kiasi kingine cha shilingi bilioni 14
zinazotokana na mchango wa Kampuni hiyo kwa Serikali ambapo inatoa
shilingi bilioni 1 kila mwezi kuanzia mwaka jana na itakuwa ikifanya
hivyo katika kipindi cha miaka mitano ambapo jumla ya shilingi bilioni
60 zinatarajiwa kupatikana.
Bw. James
alizitaka Kampuni na Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa kuiga
mfano wa Kampuni ya Airtel ili fedha zinazopatikana zichangie shughuli
mbalimbali za maendeleo ya nchi ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya
maendeleo, kuboresha huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji kwa
Watanzania wote.
“Mashirika ya
Umma na Kampuni ambazo bado zinatoa gawio dogo na zile ambazo hazitoi
gawio, zinatakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinafanya vizuri na kulipa
gawio ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo”,
alisisitiza Bw. James
Naye Msajili wa
Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka alisema ofisi yake imeendelea kuweka
mikakati madhubuti kuhakikisha Taasisi, Mashirika ya Umma na kampuni
ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa tija na zinaendelea kutoa
gawio endelevu kwa Serikali.
Awali, Msajili wa
Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka aliipongeza Airtel Tanzania Plc kwa gawio
na mchango wake wa maendeleo na kuitaka kuendelea kudhibiti matumizi na
kuimarisha teknolojia katika utoaji wa huduma.
Aliahidi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni zote ambazo Serikali ni
mwanahisa na kwamba wasiridhike na gawio walilotia bali mwakani watoe
kiwango kikubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi.
No comments :
Post a Comment