Wednesday, September 30, 2020

Mtumishi TRA aangua kilio baada ya makachero wa TAKUKURU kumnasa na milioni 8,000,000/-



Stacks of Tanzanian Shilling notes. PHOTO|FILETaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) mkoani Mwanza imemkamata Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi.Mary Moyo (34) kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na Kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Daudi Ndyamukama amesema, Bi.Moyo aliomba rushwa ya shilingi milioni nane kutoka kwa mfanyabiashara ili aweze kumrekebishia hesabu zake na kumtengenezea 'control number' ya deni analodaiwa ambalo baada ya kumpatia rushwa hiyo angempunguzia deni kutoka sh.milioni 97,156,994 hadi kufikia sh.milioni 35,000,000.

Awali ilidaiwa kwamba, kwa nyakati tofauti mfanyabiashara huyo aliambiwa kuwa anadaiwa kiasi kikubwa cha deni la kodi ambacho hakuwa na kumbukumbu ya deni hilo. Baadae alipewa barua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania inayoonyesha kuwa ana deni la sh.milioni 97,156,994.

"Hata hivyo, afisa huyo wa TRA alimshawishi mfanyabiashara huyo alipe kiasi cha shilingi milioni 35 kwa makubaliano kwamba kati ya kiasi hicho cha fedha Afisa atapewa za kwake shilingi milioni nane ili amtengenezee deni la shilingi milioni 27 ambalo angelipa kwa control number.

"Taarifa za uwepo wa tukio hili la rushwa zilifikishwa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza na mara moja tulianzisha uchunguzi. Mnamo Septemba 26,2020 siku ya Jumamosi, Bi.Mary Moyo alimpigia simu mfanyabiashara huyo na kumuelekea kuwa afike eneo la St.Dominic Nyakahoja Mtaa wa Balewa Kata ya Isamilo jijini Mwanza ili ampatie kitita cha shilingi milioni nane alizomuomba.

"Ndugu waandishi wa habari,rushwa hupofusha waonao, baada ya mfanyabiashara kufika eneo la tukio na kumkabidhi Bi.Mary fedha alizoomba, Mary aliipokea na kuweka kwenye begi la kompyuta. Mara baada ya Mary kupokea fedha hizo za rushwa, ghafla maafisa wa TAKUKURU walifika katika eneo hilo na kumuweka chini ya ulinzi. Bi.Moyo alipogundua kuwa amekamatwa na maafisa wa TAKUKURU aliangua kilio huku akiomba kusamehewa.

"Uchunguzi wa tuhuma hii umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani leo Jumatano Septemba 30,2020 kujibu mashtaka yanayomkabili.

"Aidha, tunampongeza mfanyabiashara huyu mzalendo ambaye ametimiza wajibu wake wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, kwa kutoa taarifa iliyofanikisha kukamatwa kwa afisa huyo anayeenda kinyume na maadili ya kazi yake.

"Tunaendelea kuwahimiza wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza wasikae kimya wanapoona au hata kuhisi uwepo wa vitendo vya rushwa, bali wawe tayari kukemea vitendo vya rushwa pindi vinapojitokeza kwa kutoa taarifa TAKUKURU,"amefafanua Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Daudi Ndyamukama.

 

No comments :

Post a Comment