Sunday, September 27, 2020

Mamilioni ya fedha za madini kutoka GGML yapeleka magari ya umeme Geita

Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita imesaini mkataba baina yake na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutengeneza magari yanayotumia umeme badala ya mafuta kuanzia mwezi Oktoba, mwaka huu hadi kukamilisha magari hayo ifikapo Februari, mwaka 2021,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mkataba huo umesainiwa leo Septemba 26, mwaka huu katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Jengo la Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji Kiuchumi (EPZA) mjini Geita.
Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Rashid Muhaya (kushoto) na Profesa William Anangisye ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (kulia) wakisaini mkataba wa kutengeneza magari yanayotumia umeme.Waliosimama ni wanasheria kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.(Robert Kalokola/Diramakini).

Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome,Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel.
Makatibu Wakuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu wa Sheria na Katiba, Profesa Sifuni Mchome,Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, Rashid Muhaya ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Geita na Profesa William Anangisye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika picha ya pamoja baada ya kusaini mkataba huo leo Septemba 26,2020. (Robert Kalokola/Diramakini).

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Kaimu Mkurugenzi Rashid Muhaya amesema kuwa, halmashauri hiyo imetenga fedha sh.milioni 50 kutoka fedha za huduma kwa jamii (CSR) kutoka Mgodi wa kuchimba Dhahabu wa Geita (GGML) kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa kutengeneza magari yanayotumia umeme.

Amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel kwa kusimamia kwa ukaribu mpango huo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuwa tayari kuingia makubaliano hayo kwa ajili ya kutengeneza magari hayo.

Mtaalamu wa Magari hayo, Dkt.Simon Marandu ambaye ni Meneja wa Kitivo cha Ubunifu na Uhuishaji wa Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema, chuo hicho kimeanzisha teknolojia hiyo mpya kwa Tanzania ambayo itatumia betri za kuchajiwa.

Amesema kuwa, magari hayo yatakuwa na uwezo wa kudumu kwa muda wa miaka kumi , lakini mfumo wake wa betri utakuwa na uwezo wa kudumu miaka mitano.

Dkt.Marandu ameongeza kuwa, magari hayo ni rafiki kwa mazingira kwa sababu hayatumii mafuta kwa ajili ya kuchafua mazingira.

Amesema, watatengeneza modeli mbili za magari ambayo modeli moja ni kwa ajili ya kutumiwa na polisi katika shughuli za ulinzi lenye uwezo wa kubeba abiria wawili.

Modeli nyingine ni kwa ajili ya kubeba abiria watano ambalo litatumika kufanya kazi ya kubeba abiria.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye amesema, chuo hicho kitazingatia masharti yote yaliyopo kwenye mkataba huo ili kutengeneza magari hayo.

Profesa Anangisye ameomba mikoa mingine nchini kuiga Mkoa wa Geita ili kutumia chuo hicho katika shughuli mbaliembali za ubunifu kwa maslahi ya nchi.

Moses Rusesa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa GGML amesema, mgodi huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Afisa Mahusiano wa GGML, Moses Rusesa akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini mkataba wa kutengeneza magari yanayotumia umeme badala mafuta kati ya Halmashauri ya Mji wa Geita na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Septemba 26,2020. (Robert Kalokola/Diramakini).

Ameongeza kuwa, GGML inafurahi kuendelea kuona fedha zinazotolewa zinatumika vizuri na kwa maendeleo ya jamii nzima hasa wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema mradi huo wa kutengeneza magari ya umeme utasaidia kutengeneza ajira kwa watu wengi ambao watahusika katika mnyororo wa matengenezo ya gari hilo.

Amesema kuwa, mradi huo unasadifu mawazo ya Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Baba Wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyetaka ubunifu wetu kuheshimiwa,kuthaminiwa na kupewa nafasi hata kama haujawa mkubwa sana.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Riziki Shemdoe amesema Geita ni mkoa wa kwanza nchini ambao umethubutu kutumia mamlaka za serikali za mitaa kuingia mkataba na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa, wizara hiyo itakuwa tayari muda wowote kusaidia halmashauri hiyo itakapohitaji msaada wa aina yoyote katika mradi huo wa magari ya kutumia umeme.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila ameziomba taasisi kutumia maprofesa kugundua vitu mbalimbali ambavyo vinasaidia jamii moja kwa moja.

Amesema, ni vizuri msomi akatunukiwa uprofesa akiwa amegundua jambo au kitu cha kuleta manufaa kwenye jamii kuliko kutunuku kwa njia ya kuandika maandiko ya tafiti tu.

Halmashauri ya mji wa Geita inaendelea kuweka rekodi ya kuibua miradi mikubwa ya maendeleo kwa kutumia fedha za CSR kutoka GGML kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017.

Moja ya miradi mikubwa ni soko kubwa la Katundu,mradi wa vibanda vya biashara jengo la ghorofa moja, kijiji cha maonyesho na sasa mradi wa kutengeneza magari yanayotumia umeme badala ya mafuta.

 

No comments :

Post a Comment