Mkutano maalum wa
mashauriano ukiongozwa na Mheshimiwa Balozi Nyamanga kwa upande wa
OACPS (kulia) na Mheshimiwa Waziri Muller akiongoza ujumbe wa Ujerumani
(kulia).
Mhe. Balozi Nyamanga akiendesha
kikao hicho cha mashauriano. Kulia ni Balozi wa Togo Mhe. K. Mbeou
na kushoto ni Katibu Mkuu wa OACPS Balozi Dkt Chikoti.
…………………………………………………………………
Jumuiya ya nchi za Afrika,
Carribean na Pacific (OACPS) imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuondoa
vizuizi vya kusafiri (travel bans) kwa baadhi ya nchi za OACPS hususan
zile zilizoonesha kuwa salama zaidi dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa
Corona kama
Tanzania. Wito huo ulitolewa katika kikao maalum cha
mashauriano baina ya Jumuiya ya nchi za OACPS na nchi ya Ujerumani
ambayo kwa sasa ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya.
Mashauriano hayo yaliyofanyika
tarehe 9 Septemba 2020 katika Ofisi za Jumuiya ya OACPS, Brussels nchini
Ubelgiji, yaliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS walioko Brussels, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na ujumbe wa Ujerumani uliongozwa na Waziri wa Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Gerd MÙLLER.
Katika kikao hicho wajumbe
walisisitiza umuhimu wa Umoja wa Ulaya kuendelea kuunga mkono Shirika la
Afya Duniani (WHO) katika kusimamia ithibati za tafiti za chanjo za
ugonjwa wa Corona na Shirika hilo kuendelea kujengewa uwezo wa kusimamia utaratibu wa kuhakikisha kuwa chanjo itakayothibitika inawafikia mataifa yote kwa usawa na kwa gharama nafuu.
Kikao hicho kilijadili pia hatua
mbalimbali zinazopaswa kuongeza msukumo kwa Umoja wa Ulaya katika
kuzisaidia nchi za OACPS kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana
na ugonjwa wa Corona hususan katika sekta ya utalii na
kilimo. Mikakati iliyojadiliwa ni
pamoja na ile inayolenga kupunguza, kufuta au kubadilisha masharti ya
ulipaji wa madeni ya nchi za Jumuiya ya OACPS na wito wa nchi za OACPS
kuutaka Umoja wa Ulaya kusogeza mbele utekelezaji wa baadhi ya kanuni na
taratibu mpya za biashara zilizopangwa kuanza kutumika mwanzoni mwa
mwaka ujao ili kuzipa nafasi nchi za OACPS kujipanga zaidi kabla ya
kuanza kutumia kanuni hizo.
Kupitia mashauriano hayo, pande
zote mbili zilitathmini mwenendo wa majadiliano ya Mkataba mpya wa ubia
wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya OACPS na Umoja wa
Ulaya yanayoendelea hivi sasa baada ya mkataba wa sasa kufikia kikomo
mwezi Desemba 2020. Pande mbili zilijadili kwa kina namna ya
kushirikiana katika maeneo yanayolenga kuongeza mnyororo wa thamani ya
mazao ya kilimo, uwiano ulio sawa katika biashara na maendeleo ya
teknolojia katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu.
Kikao kilihitimishwa kwa Ujerumani
kuonesha utayari wa kuyapa kipaumbele masuala yote yaliyojadiliwa
katika kipindi cha uongozi wake wa Baraza la Umoja wa Ulaya na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi
hiki ambacho inashika nafasi ya Rais wa Baraza la Mawaziri wa nchi 79
wanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific itaendelea
kushirikiana na Umoja wa Ulaya na kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa
Ujerumani kwenye Baraza la Umoja huo wa Ulaya kusukuma ajenda zenye
manufaa na maslahi kwa pande zote mbili.
No comments :
Post a Comment