Saturday, September 26, 2020

Je una mpango wa kustaafu kwa hiyari au kwa lazima?

Mpango wa kustaafu ni uthibitisho ambao unatatanisha sana miongoni mwa wafanyakazi wengi, uliyojaa vitu vyenye mashaka na visivyotabirika na kuaminika

Na Christian Gaya

Majira Ijumaa  18 Septemba.2020

Pensheni ya hifadhi ya jamii ni ya muhimu sana kwa mtu yeyote anayetegemea kustaafu kazi kutokana na kazi ya kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe. Ni mtu mwenyewe anaweza kusimamia sababu zinazoweza kujenga au kubomoa utaratibu wa pensheni ya hifadhi ya jamii.

Kwa msingi kamili wa pensheni ni uhakika kuwa mtu atakuwa na utaratibu wa fulani wa kusimamia katika miaka yote atakayokuwa kazini na kuhakikisha kuwa mwajiri wake anapeleka michango yake katika ofisi ya hifadhi ya jamii fulani pale alipo kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi sehemu za kazi na kuhakikisha kuwa anajua hata jinsi ya kukokotoa pensheni yake na mafao mengine ya muda mfupi.

Ni mtu mwenyewe anatakiwa kujua ya kuwa katika hifadhi ya jamii je kuna kustaafu mapema na ukistaafu mapema yaani kabla ya kufikisha umri wa kustaafu unaweza kupata pensheni pungufu na kiasi gani na baada ya miaka mingapi. Vile vile lazima ujue kama hiyo pensheni yako inakatwa kodi ya makato au hayakatwi. Na kama inakatwa kodi ya mapato ni kiasi gani yatakuwa yamepunguza pensheni yako na kwa miaka mingapi.

Utafiti unaonesha ya kuwa mfanyakazi mwenye afya kamili inayotakiwa katika muda wake wa kuajiriwa inatakiwa afanye kazi kwa muda wa usiozidi miaka 30 ili kupata kunufaika hadi mwisho na fao linalotakiwa katika maisha yake. Hapa tunachukulia ya kuwa ameanza kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 30.

Unapoamua ni lini unataka kuanza kupata pensheni yako, kama mwanachama mchangiaji unatakiwa kujua vipengele muhimu pamoja na mahitaji ya haraka ya mapato yako, upatikanaji na kiwango cha rasilimali zingine za kustaafu, na maamuzi mengine kama utaendelea kufanya kazi au hapana.

Kama huna sababu ya mahitaji ya haraka ya kutumia michango yako ya pensheni, itakuwa ni maamuzi ambayo siyo ya busara kabisa kuanza kutumia michango yako ya pensheni wakati bado unafanya kazi.

Madhara makubwa ya kudumu ya kuwahi kustaafu mapema ni kuwepo na kupunguziwa na mafao yako ya pensheni ambayo ungeweza kupata pensheni bora zaidi kama ungeamua kuendelea kufanya kazi mpaka unapofikisha umri wa kustaafu, na pengine ni kukatwa kwa kodi ya mapato kwenye mafao ya pensheni yako. Kwa kufanya hivyo inasababisha kupunguza sana mafao ya pensheni halisi ambayo ulitakiwa uyapate hata kwa wafanyakazi wenye mapato wastani ya mwaka.

Lakini kwa upande mwingine inaweza kuwa ni vizuri zaidi kuwahi kustaafu mapema kama unataendelea kujipatia kipato zaidi kwa kujiajiri wewe mwenyewe na wakati mwingine unaweza ukajikuta unapata kipato kikubwa zaidi ya kile ulichokuwa unapata ulipokuwa umeajiriwa kuliko kusubiri kustaafu mpaka utakapofikisha umri wa lazima wa kustaafu.

Kwa kutumia sayansi ya kijamii, inaonesha ya kuwa mchanganuo wa wastani wa matarajio ya muda wa kuishi wa binadamu, unasema kuwa mtu mwenye miaka chini ya wastani wa matarajio ya kuishi au wenye kiwango cha juu cha mapunguzo ya mafao ya pensheni ni bora akaanza mapema kuchukuwa mafao yake.

Na mtu mwenye matarajio ya kuishi maisha mengi zaidi ya wastani ya miaka ya kuishi anatakiwa kuahirisha mafao ya pensheni yake mpaka atakapofikia umri wa kustaafu kwa hiyari au kwa lazima

Mpango wa kustaafu ni uthibitisho ambao unatatanisha sana miongoni mwa wafanyakazi wengi, uliyojaa vitu vyenye  mashaka na visivyotabirika na kuaminika juu ya kiasi gani cha fedha kitachohitajika wakati wa kustaafu na mambo mengine kama vile jinsi ya kujua kiwango cha kuchangia kwenye mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii, na kiasi gani cha rasilimali ya kustaafu kinatakiwa kuwekezwa kwenye vitega uchumi, na kiasi gani cha michango au mafao kinachotakiwa kutoa kutoka katika rasilimali ya kustaafu au kutoa kabla ya kufikisha miaka ya kustaafu kulingana na mujibu wa sheria.

Ikumbukwe ya kuwa matokeo ya kufanya maamuzi mabaya mara nyingi huwa inapunguza rasilimali za kustaafu na kusababisha kiwango cha kuishi kwa mstaafu kupungua au kuhitajika kuchelewesha muda wa kustaafu ili kukusanya rasilimali ya ziada kwanza. Kimsingi kunahitaji kutoa maamuzi yenye busara ya hali ya juu ili kupata njia nzuri ya kujua mchanganyiko huu wa hifadhi ya jamii, pensheni zinazotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii au pensheni zinazoweza kutolewa na mwajiri, mpangagilio wa rasilimali za mtu binafsi, hatifungamani, hesabu ya soko la fedha na hisa, na jinsi ya kumiliki nyumba vinaingiliana na jinsi ya kuamua juu ya rasilimali iliyopo na matumizi ya pensheni za kustaafu.

Mara kwa mara baadhi ya maswali ya msingi ambayo wafanyakazi vijana na wafanyakazi wazee wanaweza kuwa nayo hasa pale wanapokaribia kustaafu ni kama vile; ni lini au wakati gani ninatakiwa kuanza kupokea mafao au pensheni ya hifadhi ya jamii? Ni thamani ya kiasi gani cha pensheni kwa kila mwaka mmoja unaongezeka kuendelea kufanya kazi na kuchangia michango baada ya kuzidisha mwaka wa lazima wa kustaafu? Ninahitaji kuendelea kufanya kazi na kuanza kupokea mafao au pensheni ya hifadhi ya jamii? Nitapata pensheni ya kiasi gani ya mkupuo na ya kila mwezi? Nitabaki kuishi mjini au itanibidi kurudi kijijini? Nitapunguza idadi ya marafiki au wataongezeka? Na kikokotoo cha pensheni kabla ya kufikisha umri wa kustaafu au baada ya kufikisha umri wa kustaafu kikoje? na maswali mengineyo mengi tu.

Kwa kiwango cha chini uchambuzi wowote unahitaji kufikiria nyongeza ya mafao ya muda wa kustaafu ukilinganisha na kodi ya mapato na kusahau ongezeko la kiasi cha pensheni kinachoongezeka baada ya mwaka wa lazima wa kustaafu. Kumbuka ya kuwa kila mwaka mmoja unaozidi mwaka wa kustaafu wa lazima unavutia kukuongezea pensheni ya asilimia 1.3 kwa wastani ya mapato yako ya kila mwezi.

Na unapoamua kutoa michango mapema kabla ya kufikia muda wa lazima wa kustaafu unapunguza asilimia 0.3 ya wastani ya mapato yako ya kila mwezi. Kuna haja kubwa ya kuchambua kwa makini sababu zinazoadhiri pensheni yako na maamuzi kamili ya kuanza lini kutumia pensheni au mafao yako ya hifadhi ya jamii

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, Mshauri na Mtaalamu wa masuala ya Pensheni na Kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com +255 655 13 13 41, unaweza kutembelea www.hakipensheni.blogspot.com, info@hakipensheni.co.tz

 

No comments :

Post a Comment