Friday, September 4, 2020

IFAHAMU HOTELI KONGWE ZAIDI ULIMWENGUNI, ILIANZA MWAKA 705




Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

HOTELI Inayofahamika kwa jina la Nishiyama Onsen Keiunkan iliyopo Yamanashi, nchini Japan inaelezwa kuwa ndio hoteli kongwe zaidi ulimwenguni iliyoanza mwaka 705 na inatambulika na kushikilia rekodi ya Guinness World Record kwa kuwa hoteli kongwe zaidi ulimwenguni kwa tuzo iliyotolewa mwaka 2011.

Hoteli ya Nishiyama imepakana na milima ya Akaishi na imekuwa ikitoa huduma tangu kuanzishwa kwake mwaka 705 na Fujiwara Mahito ambaye alikuwa mtoto wa msaidizi wa mfalme wa 38 wa Japan (Mfalme Tenji,) na imepita mikononi mwa wa vizazi 52 vya familia hiyo katika uendeshaji wake kwa zaidi ya miaka 1,300.

Upekee wa hoteli hii unatokana na chemchem zinazotiririsha maji ya moto kutoka milima ya Akaishi na Hakuko tangu kuanzishwa kwake, ambapo iliaminika kuwa maji hayo yanaponya hivyo iliwavuta watembeleaji wengi zaidi.

Ukarabati mkubwa wa hoteli hiyo ulifanywa mwaka 1997 lakini walihifadhi mtindo wa asili wa hoteli hiyo huku iliyoweka rekodi ya kutembelewa na watu maarufu na kihistoria wakiwemo Takeda Shingen na Tokugawa Leyasu.

Hoteli ya Nishiyama ina  jumla ya vyumba 37, mgahawa, maji ya moto yatokayo moja kwa moja katika chemchem za Hakuko na sehemu ya kuangalia mawio na machweo ya jua na hakukuwa na huduma ya mtandao eneo hilo hadi ilipofika mwaka 2019 ambapo huduma za mtandao (Free WiFi,) ziliunganishwa katika kila chumba cha hoteli.

No comments :

Post a Comment