
………………………………………………………………………..
Na Shamimu Nyaki – WHUSM
Sekta ya Filamu nchini imeendelea
kuwa mhimili katika ukuaji na maendeleo ya uchumi wa
watanzania na Taifa
kwa ujumla. Sekta hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha na
kuendeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda ambao umeifanya Tanzania nchi ya
Uchumi wa Kati.
Serikali kupitia Bodi ya Filamu
imeendelea kuhakikisha wanatasnia wa Filamu wanashiriki vyema katika
kufikia azma hiyo kwa kutengeneza ajira, mapato na kuchangia maendeleo
ya sekta nyingine kama vile utalii, uchukuzi na usafirishaji.
Bodi ya Filamu imeendelea
kuhakikisha kuwa maudhui ya filamu zinazopelekwa katika masoko ya ndani
zilizotayarishwa na watengenezaji kutoka ndani na nje ya nchi
zinahakikiwa na kuzipangia madaraja kwa ajili ya kuzingatia taratibu za
kisheria kabla hazijapelekwa sokoni au kwa walaji kupitia mifumo na njia
mbalimbali.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya
Filamu Dkt. Kiago Kilonzo kupitia semina na warsha mbalimbali alizotoa
kwa wadau wa sekta hiyo anasema yapo mambo mbalimbali ambayo yameleta
mafanikio makubwa katika tasnia hii ambayo yameleta tija kwa wadau na
taifa kwa ujumla.
Mafanikio hayo ni pamoja na
ongezeko la vibali vya utayarishaji wa filamu ambapo kuanzia mwaka wa
fedha 2015/2016 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2019, Vibali 620
vilikuwa vimetolewa. Kati ya vibali hivyo, vibali 480 vilitolewa kwa
watengenezaji kutoka nje ya nchi na vibali 140 kwa watengenezaji
watanzania.
“Katika Awamu ya Tano jumla ya picha
jongevu (filamu) zilizohakikiwa zimeongezeka kutoka filamu 1331 kwa
mwaka 2015/2016 hadi filamu 3,620 kwa mwaka 2019/2020 hadi mwezi Mei,
2020. Kati ya filamu hizo, filamu 3079 zilikuwa za watayarishaji wa
ndani kitanzania na filamu 541 kutoka nje ya nchi” alisema Dkt.Kilonzo.
Hata hivyo, Bodi ya Filamu
imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha utendaji katika sekta hii ikiwa
ni pamoja na kurasimisha shughuli na biashara za filamu ikiwemo
miundombinu ya usambazaji, utayarishaji na uoneshaji wa Filamu. Aidha,
utaratibu wa kuwatambua waigizaji, waandishi wa miswada, watayarishaji,
wachekeshaji, waongozaji na wasambazaji unaendelea kwa kuwapatia
vitambulisho vinavyotolewa kwa kuzingatia kada zao.
Mathalani kupitia wadau mbalimbali
wakiwemo DSTV, AZAM Media, Kampuni ya Steps Entertainment, Pilipili
Entertainment wamekuwa mstari wa mbele kutoa ajira kwa wasanii wengi
kupitia miradi ya utayarishaji wa tamthilia mbalimbali. Baadhi ya
tamthilia hizo ni pamoja na Kapuni, Huba, Slay Queen, Nyavu, Sarafu,
Tandi, Single Mama, Shiingi, Panguso na Uhuru una gharama zake.
Katika kutekeleza majukumu yake,
Bodi imeendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wake ikiwemo Vyama na
Mashirikisho mbalimbali ya watendaji na wadau wa Sekta ya Filamu nchini
hatua iliyosaidia kuimarisha Miongozo ya Vyama hivyo na kuwezesha
upatikanaji wa Katiba ya Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) iliyofanyiwa
marekebisho ili kuongeza tija na uwajibikaji kwa maendeleo ya sekta.
Ni wazi maboresho yaliyofanyika
yametoa dira imara inayoijenga na kuiimarisha sekta ya Filamu, ni wakati
sasa kwa wasanii kuona fursa zilizopo katika tasnia hiyo na kutengeneza
kazi bora ambazo zintaendana na soko la Dunia ya leo.
MWISHO.
No comments :
Post a Comment