Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sabra Machano. (Na
Mpigapicha Wetu)
Na Christian Gaya, Majira Ijumaa
11.Septemba.2020
Utafiti wa hivi karibuni
unaonesha ya kuwa wastaafu wengi nchini huishi maisha ya dhiki muda mfupi tu
baada ya kupokea mafao yao kutoka katika mifuko ya pensheni ya hifadhi ya
jamii. Pia utafiti huo unaonesha ya kuwa idadi kubwa ya wastaafu hawa huingia kwenye matumizi mabovu ya fedha pindi wanapopata malipo yao ya kustaafu kwa mkupuo na baadaye kubakiwa na malipo ya pensheni ya kila mwezi ambayo ni pensheni ndogo sana ambayo haiwezi kukidhi mahitaji yao ya lazima na familia zao.
Malipo ya pensheni kwa
wastaafu mara nyingi huingizwa kwenye matumizi mabovu na kwenye uwekezaji
usiokuwa na uzoefu wa kuleta tija yeyote.
Wastaafu
wengi wamekuwa wakihangaika kujikimu wakitegemea malipo yao ya pensheni ndogo
ambayo hutolewa kila mwezi. Fedha za malipo ya pensheni tu haziwezi kukidhi
mahitaji yao ya lazima kimaisha kama kusomesha watoto, gharama za matibabu
na kuanzisha miradi ya kujiendeleza. Matokeo yake wastaafu wengi wamekuwa
wakiishi kwa kuunga unga tu bila ya kuwa na vyanzo vya fedha vyenye uhakika.
Na
ndiyo maana mpango wa kupatiwa mikopo wastaafu kupitia Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii wa Zanzibar (ZSSF) ulioanzishwa na ZSSF kwa kushirikiana na benki ya
posta tanzania (tpb) umekuwa ukombozi mkubwa kwa wastaafu nchini kwa kukuza
uchumi wao binafsi na kuongeza pato la Taifa kwa ujumla.
Mpango huu
unaojulikana kama 'Wastaafu Loan' na unalenga kukidhi mahitaji halisi ya fedha
kwa wastaafu kwa kuwapa mikopo ya matibabu, ada za shule, kuendesha biashara na
miradi mbalimbali.
Utafiti
uliofanywa hivi karibuni unaonesha kuwa wastaafu wanaingiza kiasi kikubwa cha
fedha katika uchumi kutokana na mafao wanayolipwa, ambapo kama watawekewa mfumo
mzuri wanaweza kujiinua kiuchumi
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mfuko wa ZSSF,
Sabra Issa Machano anasema,
wastaafu wanaweza kuchangia uchumi kama vile kuongeza uwezo wa kifedha kwa
wajasiriamali mbalimbali nchini kwa kununua bidhaa zao na katika taasisi za
kifedha, kuongeza ajira, kukuza kipato, na hivyo kupunguza umaskini na pia
katika kudumisha utulivu nchini.
Anasema,
kabla ya mpango huu, wastaafu wa ZSSF walikuwa hawana fursa ya kupewa mikopo
kutokana na ama taasisi za fedha kuwa na hofu ya usalama wa mikopo yenyewe, kwa
imani kuwa wastaafu ni wazee, hawana umri mrefu wa kuendelea kuishi tena au
wakati mwingine kwa wastaafu wenyewe kutokuwa na elimu ya kuendesha miradi
inayoweza kuwapatia faida na kurejesha mikopo hiyo.
“Na
hivyo taasisi za hifadhi ya jamii, taasisi za fedha pamoja na wataalam wa
uwekezaji wanatakiwa kubuni njia na mipango ya kuwasaidia wastaafu ambao
wana kiasi kikubwa cha fedha kitakachoweza kuchangia maendeleo ya Tanzania,”
Machano anakumbusha.
Hasan
Khamis ambaye ni mkazi wa Jumbi ni mmojawapo wa wastaafu wanaonufaika na mpango
huu wa “wastaafu loan” anatoa ushuhuda wa kuanzisha shughuli zake za kuendesha
kilimo maeneo ya Jumbi Mkoa wa Kusini Unguja na mstaafu wa mwaka 2015.
“Kwa
sasa nina mpango wa kutaka kuongeza kukopa zaidi ili niweze kununua gari ndogo
ya mizigo ili kustawisha biashara zangu zaidi, kwa kweli ZSSF ni ufunguo wa
maisha”mzee Khamis anasema.
Tangu
mpango huu uanzishwe mwaka 2014 yaani miaka mitatu iliyopita umeshawanufaisha
zaidi ya wastaafu wapatao 500.
“Lengo
la kuanzisha mpango huo ni kuwajali wanachama wetu hata wakiwa katika ustaafu
wao na hiyo inakwenda sambamba na kauli mbiu yetu ya ‘ZSSF’ ni ufunguo wa
maisha,”Machano ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa ZSSF anasema.
Mikopo
hii inawasaidia wastaafu kujikwamua kiuchumi na kuweza kuishi maisha bora au
pengine zaidi ya yale waliyoishi kabla ya kustaafu na miongoni mwa mahitaji
makubwa ya fedha za wastaafu ni gharama za matibabu, ada ya shule, kuendesha
biashara au miradi mbalimbali na wakati huo huo mstaafu anapata nafuu, kwani
ataendelea kupata pensheni yake kama kawaida huku akiendelea kulipia deni la
mkopo.
“Tunauona mpango huo ni ukombozi mkubwa kwa
wastaafu, kinachotakiwa ni kwa wastaafu kupewa mafunzo ili kuwawezesha na
kuwashauri namna bora ya kuwekeza na miradi ipi ya kufanya ambayo haina hasara
kubwa wala shinikizo,”anafafanua zaidi.
Anasema,
mkopo huu unawasaidia wastaafu kwani hauna dhamana na kuongeza kuwa mkopaji
anaweza kukopa kuanzia shilingi 500,000/= hadi milioni 20 kwa kiwango cha riba
kilicho chini ya kile kinachotolewa katika soko na taasisi zingine za kifedha
nchini, zinazolipwa kupitia pensheni yake ya mwezi ndani ya mwaka mmoja hadi
mitatu.
Na faida nyingine ya mstaafu loan, ni pale
mstaafu anapokuwa na fursa ya kuongeza kukopa hata kama hajamaliza mkopo wake
ili mradi anamwendelezo mzuri wa kulipa mkopo wake. Na mstaafu
anayehitaji mkopo hahitaji kuwa na dhamana, kwani mkopo huo una bima na endapo
mkopaji atafariki familia yake haitadaiwa
Machano
anasema mkopo huu ambao ni wa kwanza katika soko la mabenki nchini, umeshaanza
kuwanufanyisha kwa kuwawezesha wastaafu kuanzisha na kuendeleza biashara zao na
kutimiza malengo yao na kujiongezea kipato.
“Hili
litamwondoa mstaafu kwenye uwezekano wa kuwa tegemezi kwa ndugu au watoto, pia
kumwezesha kuchangia kwenye uchumi wa nchi yetu,” anasema.
Anasema mpango huu wa utoaji wa
mikopo kwa wastaafu una lengo la kuleta faraja na kuwasaidia wastaafu katika
kukidhi mahitaji yao mbali mbali ya kimaisha ikiwamo kulipia gharama za
matibabu, ada za shule za watoto au wajukuu na kuendesha biashara ndogo ndogo
zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya kila siku.
Machano anafafanua ya kuwa nia yao ni kujenga mazingira mazuri kwa
wastaafu walio wanachama wa ZSSF ili kustaafu kusiogopwe na kuonekana ni mwanzo
wa kuanza kwa kipindi cha maisha ya shida yasiyokuwa na matumaini.
“Tunataka kujenga tabia ya kuwafanya
wafanyakazi wanapopata barua za kustaafu wasihuzunike kama ilivyozoeleka,”
anadokeza na kusema ya kuwa mwanachama wa ZSSF anayetaka mkopo anatakiwa aende
kwenye tawi lolote la benki ya tpb ililopo karibu naye ili kupata huduma
Machano anasema.
Christian
Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala
ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com +255 655 13 13 41, unaweza kutembelea www.hakipensheni.blogspot.com, info@hakipensheni.co.tz
No comments :
Post a Comment