Thursday, August 13, 2020

World vision yatoa magodoro 100 na vitanda 50 kuboresha elimu ya mtoto wa kike.


Na Samirah Yusuph
Shule ya sekondari Simiyu ni miongoni mwa shule nufaika na mikakati inayofanywa na shirika lisilo la kiserikali la world vision, ambapo jana imepokea msaada wa vitanda 50  (double decker) pamoja na magodoro 100.

Akikabidhi vitanda hivyo kaimu meneja wa krasta ya Nzega  Gilselda Balyagati alisema, Kupitia mradi wa KANADI shirika limeweza kutoa milioni 26.6 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa linamtengenezea mtoto wa kike mazingira mazuri ya kupata elimu.

"Lengo la shirika ni kuwalinda wasichana dhidi ya vishawishi pamoja na mimba na ndoa za utotoni na kuhakikisha kuwa wanapata elimu bora," alisema  

Aliongeza kuwa, wanaishukuru serikali kwa ushirikiano inao utoa kwa mashirika binafsi na wadau wengine wa maendeleo hali inayowafanya wasichoke kuunga mkoa sera ya serikali ya hapa kazi tu.

Akipokea vitanda hivyo mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alisema kuwa, ni wakati wa wanafunzi kutumia fursa wanazosogezewa na serikali kwa ajili ya manufaa yao na kiacha kucheza na wakati.

"Nyinyi kazi yenu ni kusoma tu, sitarajii kuwa serikali ikufanyie kila kitu na ufeli huo utakuwa ni ujinga wako wekeza sana katika kusoma maana elimu inatolewa bure," alisema Kiswaga.

Kiswaga aliongeza kuwa licha ya upatikanaji wa wadau katika kusaidia kuboresha Elimu Walimu pia wanajukumu kubwa kuhakikisha kuwa wanafanya kazi ipasavyo ili kuwawezesha wanafunzi kifauru vizuri. 

Aidha baadhi ya wanafunzi ambao ni wanufaika wa msaada huo, wameeleza namna ambavyo wamepokea vitanda hivyo na kusema kuwa kwao ni mafanikio makubwa katika elimu.

"Ukilala vizuri lazima uamke akili yako imechangamka tumefurahi sana na sisi tunaahidi kutunza vizuri vitanda na magodoro haya ili hata wadogo zetu waweze kuyatumia hapo baadae," alisema Kwiyeya Lameck Buluba mwanafunzi wa kidato cha kwanza.

"Ni faraja kwetu tunapoona kunawatu wapo nyuma yetu ili kuhakikisha tunapata elimu bora na kulindwa dhidi ya ukatili wa kingono, tumepata vitanda vingi ambavyo vitatusaidia kuishi mazingira ya hapo shuleni ni jambo la kushukuru sana," alieleza Rita Masunga mwanafunzi wa kidato cha tatu.

Shirika la world vision Tanzania ni miongoni mwa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwenye jamii hasahasa katika upande wa Elimu na Afya.

 

No comments :

Post a Comment