WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) ihakikishe Watanzania hawarubuniwi ili watumie vizuri utashi
wao wa kisiasa kuchagua viongozi bora.
“Sote
tunatambua kuwa Oktoba, mwaka huu Taifa letu litaendesha Uchaguzi Mkuu
wa Rais, Wabunge na Madiwani… mna jukumu zito la kuhakikisha Watanzania
hawarubuniwi na msimuonee au kumpendelea yeyote kwa maslahi yenu
binafsi.”
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 12, 2020) alipofungua jengo la
Intelijensia TAKUKURU Makao Makuu Dodoma. Amewasihi watumie vizuri ofisi
hiyo kukusanya taarifa muhimu za kiintelijensia zinazowahusu wagombea,
vyama au wananchi watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi
mkuu.
Waziri
Mkuu amesema wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga
kura Oktoba 28, 2020 na kwamba wanawajibu wa kuchagua Serikali bora na
kiongozi bora atakayewaletea maendelea maendeleo. “Chagueni kiongozi
mwenye maono aliyetenda na atakayetenda.”
“Tayari
tumeshuhudia mking’ata baadhi ya wagombea waliojihusisha na vitendo vya
rushwa kwenye hatua za awali za uteuzi wa wagombea kupitia vyama vyao.
Msiache; endeleeni kukaza uzi na kuwadhibiti wote wenye kujihusisha na
vitendo hivyo,” amesisitiza.
“Niungane
pia na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuwasihi wanasiasa na
wagombea wenzangu wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu
mwezi Oktoba mwaka huu tuache kutumia rushwa kwa lengo la kununua
uongozi.”
Waziri
Mkuu amesema wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, ni vema Watanzania wote
na viongozi wakazingatia nasaha za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, katika moja ya hotuba zake alipowataka wajiulize
kwamba mgombea anayetumia rushwa kununua kura amepata wapi fedha hizo na
je, akipata uongozi, fedha hizo atazirudishaje.
Amesema:
“Kwa hivyo, nasi ifike mahala tuwahoji hawa wanaotutia doa. Je, wewe
mwenzetu unayetumia rushwa kununua uongozi umepata wapi fedha hizo? Na
je? tukikuchagua, utarejesha vipi fedha hizo? Nitoe wito kwa Watanzania
wote, msikubali kuwachagua wagombea wanaotumia rushwa ili kupata nafasi
za uongozi.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapongeza Viongozi wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na watendaji wa TAKUKURU
kwa kusimamia vema mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ndani na nje ya
Serikali.
Waziri
Mkuu amesema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa udhibiti wa
matumizi ya hovyo ya fedha za umma; imeongeza usimamizi katika
ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuziba mianya ya ukwepaji kodi.
Pia,
Waziri Mkuu amesema ni lazima wafanye uchunguzi wa kutosha juu ya
matumizi ya fedha zote za umma na kujua kama matumizi hayo yanaenda
sambamba na matakwa ya kisheria na pale ambapo watabaini ukiukwaji wa
sheria wachukue hatua.
“Nyote
mtakubaliana nami kuwa miongoni mwa mambo yaliyopewa uzito mkubwa na
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari na Rais wetu mpendwa,
Dkt. John Pombe Magufuli ni kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya
rushwa na ufisadi.”
“Rais
Dkt. Magufuli amemudu kurejesha imani ya Watanzania kwa watumishi wa
umma na zaidi ya yote amerejesha uwajibikaji. Ni ukweli usiopingika
kwamba tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kulikabili tatizo la rushwa na
ufisadi ndani ya Taifa letu.”
“Kwa
upande mwingine, mafanikio tuliyoyapata hayajajikita katika kukabili
mafisadi na wala rushwa tu, bali pia katika kuijengea uwezo wa
kiutendaji TAKUKURU. Lengo ni kuiwezesha taasisi hii itekeleze majukumu
yake kwa ufanisi zaidi. Jengo hili tunalolifungua leo, ni kielelezo
tosha cha baadhi ya jitihada hizo.”
Waziri
Mkuu amesema amefurahishwa na kitendo cha TAKUKURU kurejesha fedha na
mali za wanyonge waliodhulumiwa mauzo ya mazao yao na kutozwa riba za
kubambikiziwa na zisizolipika. “Hatua hiyo, imeudhihirishia umma kuwa
TAKUKURU sasa inang’ata kwelikweli.”
“Kama
mtakumbuka, operesheni ya urejeshaji wa fedha za wakulima zilizotokana
na mauzo ya korosho na ufuta, ilianzia mkoani Lindi na baadaye kuhamia
katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Simiyu na hatimaye nchi nzima.”
Pia,
Waziri Mkuu amesema TAKUKURU imewafuta machozi Watanzania wengi hususan
wastaafu ambao kwa kutotambua haki zao, walikopa fedha kidogo kutoka
kwa wajanja fulani fulani.
Amesema
wajanja hao, wakatumia hila kupitia makubaliano ya taratibu za mikopo
hiyo, kuwataka wakopaji warejesha kiasi kikubwa cha fedha
kilichojumuisha riba ya zaidi ya asilimia 100. Jambo hilo, si tu ni
kinyume na taratibu za ukopeshaji wa fedha bali pia ni uvunjanji wa
sheria na ni uonevu mkubwa kwa wananchi.
Ufunguzi
huo umehudhuliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Kapt. Mst. George Huruma Mkuchika, Mkurugenzi
Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo.
Wengine
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Dkt. Mary Mwanjelwa, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) Charles Kicheere, Katibu Mkuu Ikulu, Dkt. Moses Kusiluka,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge na maofisa wengine wa
Serikali.
No comments :
Post a Comment